Wekundu wa Msimbazi, Simba Sports Club wamechukua alama zote 3 kwenye Mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kuwanyuka Tabora United mabao 4-0 mchezo uliopigwa kwenye uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabira.
Mchezo ulianza taratibu huku timu zote zikisikiliziana kwenye mashambulizi kabla ya Simba kuuchukua Mchezo kuanzia dakika ya 10.
Saido Ntibazonkiza alitengenezewa nafasi na Pa Omar Jobe lakini shuti lake lilienda kugonga nguzo ya pembeni na kutoka nje.
Simba walipata bao la Utangulizi kupitia kwa Pa Omar Jobe dakika ya 19 ya mchezo akiunganisha vizuri kwa kichwa Mpira wa adhabu uliochongwa na Clatous Chama.
Makosa ya kiulinzi ya Tabora United alamnusura yaizawaidie Simba bao la 2, Clatous Chama aliunasa mpira na kuingia nao hadi kwenye 18 ya Tabora United lakini krosi yake haikuweza kumaliziwa vizuri na Saido Ntibazonkiza na kuokolewa na walinzi.
Licha ya kuonekana kuishika mechi lakini Simba walishindwa kutumia vema nafasi zao walizokuwa wakizitengeneza huku pia Tabora United wakionekana kukosa utulivu eneo lao la ulinzi hasa wakijaribu kuonesha kujiamini eneo hilo lakini kunbe wakiwaruhusu sana Simba kuwasogelea.
Dakika ya 36, Sadio Kanoute aliwaandikia Simba bao la 2 akiunganisha kwa kichwa krosi murua kutoka kwa Shomari Kapombe upande wa kulia wakati mpira ukionekana kama hauna madhara.
Clatous Chama alijitengenezea nafasi tena akiwachachafya walinzi wa Tabora United lakini shuti lake pakiwa hakuna kipa langoni lilimgonga Saidi Mbatty akiwa kwenye mstari wa goli na kukoa shambulizi hilo. Almanusura Simba wapata bao la 3 dakika ya 39 ya mchezo.
Mpaka Mapumziko Simba walienda kifua mbele kwa mabao 2-0.
Tabora United walirejea kipindi cha pili na mabadiliko kadhaa huku wakiingizwa wakiwemo Abdallah Madilisha na Yohana Mkomola lakini bado Simba walionekana kuutawala mchezo wakiendelea kuwa watulivu huku wakishambulia kwa kasi.
Alikuwa ni Che Malone alieendelea kuwanyong’onyesha Nyuki wa Tabora kwa kushindindilia msumari wa 3 akimalizia heka heka zilizoshindwa kuokolewa langoni mwa Tabora United na kupiga Shuti kali lililomshinda Kipa John Noble. Dakika ya 61, 3-0 Tabora United.
Dakika ya 87, Freddy Kouablan alifunga bao lake la kwanza tangu ajiunge na Wekundu wa Msimbazi dirisha dogo akiiandikia Simba bao la 4 akitumia jitihada binafsi kisha kupiga shuti lililotinga moja kwa moja wavuni, John Noble asiwe na la kufanya.
Dakika zote 90 zikatamatika kwa Simba kuibuka na Ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Tabora United.