Kocha mkuu wa kikosi cha timu ya Taifa ya Congo DR Sebastien Desabre amesema kwa upande wao watafanya kila kitu ili kufika fainali za mataifa ya Afrika kwenye mchezo wao wa nusu fainali dhidi ya Ivory Coast.
Congo Dr itashuka dimbani kuikabili Ivory Coast majira ya saa tano [23:00] usiku kwenye uwanja wa Stade Alassane Ouattara uliopo mji wa wa Yamoussoukro wenye uwezo wa kubeba watazamaji 60,000.
Desabre anaamini vijana wake watatoa matokeo ya kushangaza kama ambavyo walifanya kwa kumuondosha bingwa mara saba wa AFCON timu ya Taifa ya Misri.
“Tunauendea mchezo huu kwa utulivu na uvumilivu, vijana wamerejea vyema baada ya kuifunga Guinea”, Alisema.
“Tumepata siku nyingi zaidi za kupumzika kulinganisha na wapinzani wetu, hili pia linaweza kuwa na umuhimu”.
Desabre ametanabahisha kuwa nguvu ya Ivory Coast ipo kwenye kumiliki wa mpira hata kama watawakosa wachezaji wao baadhi.
“Wana kikosi bora, hata kama bila wachezaji wao wanne, wana nguvu na benchi lenye ubora”. Aliongeza.
Kocha Desabre aliweka wazi kuwa wanaweza kuathiriwa na hali ya uwanja lakini watajitoa kwa moyo wao.
“Sisi ni washindani, tunataka kufika fainali na tutafanya chochote kufanikiwa”, Desabre aliongeza.
Baada ya kuiondosha Misri na Guinea sasa timu ya Taifa ya Congo DR inatafuta kombe lake la kwanza tangu walipobeba AFCON mara ya mwisho 1974.