Makala Nyingine

DUBE AISHIKA PABAYA SIMBA IKIAMBULIA SARE KIRUMBA

Published on

Mzizima Derby imetamatika kwa sare ya bao 1-1 huku kila timu ikiambulia alama 1 kwenye mchezo wa ligi kuu Tanzania Bara uliopigwa kwenye uwanja wa CCM Kirumba. Azam wanasalia nafasi yao ya 2 wakiwa na alama zao 32 huku Simba wakifikisha Alama 30 kwenye nafasi ya 3.

Azam walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa Prince Dube dakika ya 14 ya mchezo akipokea pasi nzuri elekezi kutoka kwa Pascal Gaudence Msindo kutoka upande wake wa kushoto. Dube akiendeleza ubabe wake kwa kuifunga mara nyingi Zaidi Simba.

Simba walijaribu kujibu mashambulizi wakionekana kucheza kiutulivu licha ya kuwa nyuma kwa bao 1, wakicheza pasi na kujaribu kutengeneza mashambulizi lakini mipira mingi ilikuwa inaishia mikononi mwa golikipa Mohamed Mustapha wa Azam ambaye alikuwa kwenye kiwango kizuri.

Prince Dube alipata nafasi ya wazi wakati walinzi wa Simba wakionekana kumsahau, lakini alishindwa kutumia nafasi hiyo, golikipa Ayoub Lakred akiwahi kutokea na kuokoa shambulizi hilo.

Kwa mara nyingi tena Prince Dube, dakika ya 45+2 akapata nafasi nyingine akitumia tena kuteleza kwa mlinzi wa kati Hussein Kazi na kupiga shuti ambalo hata hivyo, Ayoub Lakred alikuwa sambamba nalo na kuiweka tena salama Simba.

Azam FC walimaliza vizuri dakika hizi 45 za kwanza wakiwa mbele kwa bao 1 lakini wangeweza kuwa mbele kwa mengi zaidi kama wangetumia nafasi zao, Simba wakiwa bado wanajitafuta huku safu ya Ulinzi na viungo wake wakabaji wakifanya kazi kubwa sana kuzuia hatari langoni mwao.

Timu zote zilirejea kipindi cha pili wakifanya mabadiliko kadhaa ya kiufundi na ya kilazima pia wakati Simba wakiwaingiza Shomari Kapombe, Kennedy Juma na Pa Omar Jobe nafasi za Israel Mwenda, Hussein Kazi na Freddy Kouablan, Azam walimtambulisha mchezoni Daniel Amoah akichukua nafasi ya Majeruhi Yahya Zayd.

Mchezo ulionekana kuwa na uwiano sawa kipindi hiki cha pili, timu zote zikishambulia kwa nyakati lakini pia wakiwa makini kwenye ulinzi kutokana na ubora wa wachezaji wa vikosi vyote viwili.

Ilibidi Simba wasubiri mpaka dakika ya 90+1 kupata alama 1, Clatous Chama alipiga mpira wa faulo ambao ulitinga moja kwa moja nyavuni na kuweka mzani sawa kuwa 1-1.

Almanusura Simba wapate bao la ushindi dakika ya 94+, Clatous Chama aliweka pasi nzuri katikati ya Pa Omar Jobe na Kibu Denis lakini walishindwa kutumia nafasi hiyo.

Mpaka dakika 90 zinatamatika, Mzizima Derby iliisha kwa sare ya 1-1, timu zote 2 zikigawana alama 1.

Baada ya mchezo Kocha wa Azam FC Youssouph Dabo alisema

Kiukweli tulistahili kushinda mchezo huu, tungeweza kuimaliza mechi mapema Kipindi cha kwanza tulikosa nafasi nyingi sana. Niliwaambia wachezaji wangu kuwa mabeki wa kati wa Simba hawak shapu sana kwenye kuzuia pasi za juu tutumie nafasi hizo na tukapata bao, yangeweza kuwa mengi zaidi Lakini dakika za mwisho tulikosa umakini na kuruhusu kusawazishiwa. Watanzania wengi hawatuheshimu ila watatuheshimu tu.

Naye mchezaji wa Simba, Shomari Kapombe alisema

Mchezo ulikuwa mgumu sana hasa pale tuliporuhusu goli la mapema lakini tuliweza kutulia na kushikilia maelekezo ya Mwalimu mpaka angalau tukaja kupata goli la kusawazisha. Sisi tunaamini kwenye kupambana mpaka dakika za mwisho na tutaendelea hivi kwenye michezo yote ijayo, hili limeisha tunajiandaa na mchezo ujao ili tutafute alama 3.

Simba wanatarajia kumaliza viporo vyao kwa mchezo dhidi ya Geita Gold utakaopigwa Jumatatu Februari 12 kabla ya kukutana na JKT Tanzania kwenye mchezo wa Raundi ya 14, Alhamisi ya tarehe 15 Februari.

Popular Posts

Exit mobile version