Makala Nyingine

GSM KUJENGA UWANJA WA YANGA JANGWANI.

Published on

Klabu ya Young Africans kupitia kwa Rais wake Eng. Hersi Said leo wametangaza kuwa mdhamini na mfadhili wa klabu hiyo Gharib Said Mohamed kupitia makampuni yake ya GSM atajitolea kushiriki kwenye ujenzi wa uwanja wa klabu hiyo.

Kwa mujibu wa Eng. Hersi ameweka wazi kuwa klabu hiyo itaanza ujenzi wa uwanja wao kwenye eneo la Jangwani ambali lipo karibu na makao makuu ya klabu hiyo.

“Baada ya mazungumzo ya muda mrefu na mfadhili na mdhamini wa klabu yetu, Gharib Said Mohamed [GSM], nipende kuwataarifa wanachama na mashabiki wa klabu yetu kuwa leo GSM ameridhia kwa dhati kushiriki kwenye kufanikisha ujenzi wa uwanja wa kisasa wa Yanga katika eneo la makao makuu ya klabu yetu Jangwani, Jijini Dar Es Salaam,” alisema Hersi.

Ni klabu tatu pekee nchini zenye viwanja vyake na klabu mbili ndizo zenye viwanja vinavyokidhi ubora wa kuchezea Ligi kuu kandanda Tanzania Bara.

Klabu hizo ni JKT Tanzania [General Isamuhyo], Singida Fountain Gate [Fountain Gate Stadium – Mwanza] na Azam fc [Azam Complex]. Ni Azam na JKT Tanzania pekee ndio zenye uwanja unaotumika kwa michezo ya Ligi kuu.

Klabu ya Yanga sasa inafikisha miaka 89 hii leo na wanaadhimisha umri huu kwenye uwanja wa Sokoine Mbeya ambapo watakuwa na mchezo wa Ligi kuu kandanda Tanzania Bara dhidi ya Tanzania Prison.

Klabu ya Yanga imekuwa na mpango wa kufanya ujenzi wa uwanja wake kwa muda mrefu sasa tangu Eng. Hersi Said aingie madarakani lakini walianza kwa kufanya maboresho kwenye ofisi zao kwanza na kuhamia hapo.

Awali shughuli za klabu zilikuwa hazifanyiki kwenye ofisi za klabu zilizopo Jangwani kwani watendaji wote walikuwa kwenye ofisi za Salamander.

Popular Posts

Exit mobile version