Nyota wa timu ya Taifa ya Ivory Coast Oumar Diakite mara baada ya kunyakua kombe la mataifa ya Afrika hapo jana anasema walikuwa kama Mizimu na sio rahisi kufa mara mbili.
“Tulikuwa kama mizimu kwenye mashindano haya, lakini sio rahisi kufa mara mbili”, Alisema Diakite.
Ivory Coast ilimaliza nafasi ya Tatu kwenye msimamo wa kundi A na kufuzu kama Bestloser na mchezo wa kwanza dhidi ya Nigeria walipoteza, wakakutana tena fainali kulipa kisasi.
Kwa upande wa kocha wa kikosi cha Ivory Coast Emerse Fae ameweka wazi kuwa ilikuwa zaidi ya maajabu kushinda taji hili.
“Kilichotokea ni zaidi ya maajabu”, Alisema Emerse Fae.
Fae alikabidhiwa timu mara baada ya kocha mkuu wa kikosi hicho kuondoshwa kutokana na matokeo mabaya waliyoyapata hatua ya makundi.
Ivory Coast ilipoteza michezo miwili [2] dhidi ya Nigeria na dhidi ya Equatorial Guinea hivyo kumaliza wakiwa nafasi ya tatu ya msimamo wa kundi hilo.
Mashindano haya yamekuwa mwendelezo wa maajabu ya timu isiyotarajiwa kunyakua ubingwa wa Bara husika kama ilivyotokea mwaka 2016 kwenye michuano ya Euro wakati Ureno inatwaa Ubingwa huo ilifuzu hatua ya 16 bora kama Bestloser na mwisho wakatwaa ubingwa.
Ivory Coast wamefanya kila kitu, wameandaa mashindano bora sana na wamejitokeza mashabiki wa kutosha kwenye kila mchezo, na hizi zinabaki kuwa fainali zilizofuatiliwa zaidi Duniani.