Nahodha wa timu ya Taifa ya Nigeria Ahmed Musa, ametoa wito kwa watu kuacha kumshambulia kiungo wa timu hiyo Alex Iwobi.
Baadhi ya mashabiki wamekuwa wakimsakama Iwobi, 27, kwenye mitandao wa kijamii, wakimlaumu kwa Nigeria kupoteza mchezo wake wa fainali ya Afcon dhidi ya Ivory Coast siku ya Jumapili.
Iwobi alicheza kwa dakika 79, kabla ya kutoka na Alhassan Yusuf kuingia.
Mashambulio ya mtandaoni yalisababisha Iwobi kufuta picha zake zote kwenye Instagram siku ya jana Jumatatu.
Nahodha wa Super Eagles, Ahmed Musa na baadhi ya Wanigeria wamemtetea Iwobi, na kulaani mashambulio hayo wakisema si haki kumlaumu mchezaji mmoja.
“Wapendwa mashabiki, naomba nitoe wito wa kuacha unyanyasaji wa kimtandao dhidi ya Alex Iwobi,” Ahmed Musa ameandika kwenye mtandao wa X.
“Kupoteza mchezo bila shaka ni jambo gumu, lakini kumshambulia mchezaji mmoja kwa jambo ambalo ni la timu nzima sio haki. Tunashinda kama timu, na tunapoteza kama timu. Alex alijtuma sana uwanjani, kama mchezaji mwingine yeyote wa kikosi chetu,” ameongeza Musa.
Iwobi mwenyewe hajasema lolote mpaka sasa kuhusu kushambuliwa huko, Nigeria walipoteza mchezo wa fainali kwa kipigo cha 2-1 dhidi ya Ivory Coast.