NBC Premier League

TABORA UNITED YAAHIDI ALAMA TATU KWA AZAM LEO.

Published on

Klabu ya Azam fc inatarajiwa kushuka dimbani hii leo kuikabili klabu ya Tabora United kwenye mwendelezo wa michezo ya Ligi kuu kandanda Tanzania Bara.

Mchezo huo unatarajiwa kupigwa majira ya saa kumi [10:00] jioni kwenye uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora, hii itakuwa mara ya kwanza kwa timu hizi mbili kukutana kwani Tabora United imepanda Ligi kuu msimu huu wa 2023/24.

Kuelekea mchezo huo kocha mkuu wa kikosi cha Tabora United Goran Kopunovic ameweka wazi ugumu atakaoenda kukutana nao mbele ya timu yenye uzoefu mkubwa kwenye Ligi ya Tanzania.

“Tunafanya kazi kubwa, kila mechi kwetu ni ngumu, kila mechi inatupa uzoefu mpya, tunacheza na Azam leo, timu kubwa ambayo ina bechi lenye uzoefu, na wachezaji wenye uzoefu”.

“Ninawaamini vijana wangu hatutaingia kinyonge kwenye mchezo huu, tunazihitaji alama tatu”, Goran Kopunovic, kocha mkuu, Tabora United.

Kwa upande wa kocha mkuu wa kikosi cha Azam Bruno Ferry yeye ameweka wazi kuwa watakutana na upinzani mkubwa mbele ya Tabora United kutokana na hali ya uwanja lakini watabadili mbinu ili waondoke na alama zote tatu hii leo.

“Tumecheza Ijumaa, tukasafiri kuja hapa kucheza na Tabora, tuna mechi nyingi sana kwa mwezi huu wa pili na hakuna muda wa wachezaji kurudisha mwili kwenye hali ya kawaida”

“Kocha ameutembelea uwanja na tutafanya mabadiliko kadhaa ya kiuchezaji kulingana na uwanja, haitakuwa vile ambavyo huwa tunacheza pale chamazi, kila timu inahitaji alama tatu”, Bruno Ferry, kocha mkuu wa Azam FC.

Afisa habari wa klabu ya Tabora United Christina Mwagala ameweka wazi kiingilio cha mchezo huo kwa mashabiki watakaopata nafasi ya kuhudhuria kuitazama timu yao ya Tabora United.

“Maandalizi yamekamilika kwa asilimia 100 kuelekea mchezo wa kesho dhidi ya Azam fc chini ya kocha Goran Kopunovic”

“Mchezo huo utapigwa saa 10:00 jioni katika uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, watanzania tunataka tuwaonyeshe kwamba tulifungwa na Azam tukiwa hatujakamilika, hivyo tunaenda kulipa kisasi tukiwa kamili”.

“Tunafahamu Azam ina wachezaji wazuri na ni timu nzuri lakini tutaenda kupambana nao, lazima wajue wanakuja kwenye vita ya kutafuta matokeo,wachezaji wote wapo kamili”.

“Kuiona Tabora United ni Shilling Elfu Kumi [VVIP], Elfu tano [VIP] na mzunguko shilling Elfu tatu [3000/=]”, Amesema Christina Mwagala, Afisa habari Tabora United.

Mchezo huo utakuwa wa kwanza kwa Azam kucheza kwenye uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora kwenye Ligi kuu kandanda Tanzania Bara.

Hadi hivi sasa Azam ipo nafasi ya tatu ya msimamo wa Ligi ikiwa na alama 35 ikicheza michezo 15, huku Tabora United ikiwa nafasi ya 14 ikikusanya alama 16 kwenye michezo 15.

Popular Posts

Exit mobile version