NBC Premier League

KIDAO: TUTAFUNGA VAR MBILI KUPUNGUZA MAKOSA YA WAAMUZI.

Published on

Katibu mkuu wa shirikisho la soka nchini Tanzania Wilfred Kidao mapema leo wakati akizungumza na EFM radio ametolea ufafanuzi juu ya kukosekana kwa waamuzi wa Tanzania kwenye michuano mikubwa kama AFCON licha ya kuwa na Ligi namba sita [6] kwa ubora Barani Afrika kwa kusema kuwa kuna kipindi shirikisho liliacha kutengeneza waamuzi.

Hata hivyo Kidao amesema kuwa tayari wamepata waamuzi ambao wameanza kuingizwa kwenye mchakato kwaajili ya kuchezesha michuano mikubwa ya AFCON 2025 inayotarajiwa kufanyika nchini Morocco mapema mwezi July hadi August.

Kuna kipindi tuliacha kutengeneza waamuzi na tumeanza kutengeneza waamuzi, kama nchi unaweza usitengeneze waamuzi wote bora lakini ukapata watatu au wanne na hata ukisikia huko wanaposema Somalia hawaendi waamuzi 20 ataenda mmoja au wawili kwahiyo kila nchi walau inatengeneza waamuzi wawili ambao wanakuwa bora.

Tumeanza kupata waamuzi ambao wameanza kuingizwa kwenye mchakato wa Afcon 2025, wakati ukifika tutaongea.

Wilfred Kidao alizungumza.

Kidao pia ametaja sababu zinazopelekea kupanda na kushuka kwa viwango vya waamuzi nchini ikiwemo matatizo ya kifamilia ambayo yanawakumba waamuzi hao, na ameweka wazi kuwa kwasasa wanaandaa utaratibu wa kuzungumza na waamuzi hao.

Kuna sababu nyingi ambazo zinasababisha mwamuzi kuonekana ameshuka, sisi kwetu huku hatuna utaratibu wa kuongea na mtu maswala ambayo yanamgusa kifamilia, kuna kipindi unaweza kumuona ni mwamuzi bora kabisa lakini maswala ya kifamilia yakasababisha atoke.

Wlifred Kidao, Katibu TFF.

Kwa upande mwingine pia Kidao ameeleza kuwa mwamuzi wa kati wa Ligi kuu kandanda tanzania Bara mwana mama jonesia Rukia alikuwa miongoni mwa waamuzi watakaochezesha fainali za kombe la Dunia zilizofanyika nchini Qatar lakini kwasababu ya matatizo binafsi [Uzazi] mwamuzi huyo hakuweza kushiriki fainali hizo na nafasi yake ikachukuliwa na mwamuzi kutoka Rwanda.

Jonesia alikuwa miongoni mwa waamuzi ambao waliorodheshwa kuchezesha kombe la Dunia la Qatar ambayo baadae akachezesha mwamuzi wa Rwanda, alikuwa na kozi nyingi kuelekea mashindano hayo lakini maswala binafsi yakasitisha.

Aliongeza Kidao.

Wilfred pia ameeleza kuwa katika kupunguza tatizo la makosa ya waamuzi nchini kuna mpango wa kufunga mitambo ya VAR miwili mmoja ukiwa kwa udhamini wa shirikisho la soka Barani Afrika CAF ambao utafungwa uwanja wa Taifa Jijini Dar Es Salaam na mwingine ukiwa wa kuhamisha.

Ili kuondoa matatizo ya kibinadamu uwanjani, hivi karibuni tutakuwa na mitambo miwili ya VAR hapa nchini, mmoja utaletwa na CAF ambao utafungwa uwanja wa Benjamini Mkapa, na mwingine mmoja ambao utakuwa wa kuhamisha na ni wa kisasa zaidi ni toleo jipya la VAR lililotolewa.

Tanzania ndio itakuwa ndio kitovu cha mafunzo ya VAR ukanda wa CECAFA [Nchi 11], itatusaidia kwa kiasi kikubwa kwasababu anaweza asiende Refa wa kati kwenye AFCON akaenda mtu wa VAR.

Alimaliza Wilfred Kidao.

Kwasasa Ligi kuu kandanda Tanzania Bara inatajwa kushika nafasi ya sita kwa kuwa na Ligi Bora Barani Afrika lakini kila kukicha zimekuwa zikiibuliwa hoja kadhaa kuhusu kukosekana kwa waamuzi kutoka Tanzania kwenye michuano mikubwa Licha ya Ligi hii kuwa namba sita kwa ubora.

Popular Posts

Exit mobile version