Azam Sports Federation

YANGA KUIKABILI POLISI TANZANIA LEO ASFC.

Published on

Klabu ya Yanga inatarajiwa kushuka dimbani hii leo kucheza dhidi ya klabu ya Polisi Tanzania kwenye mchezo wa ASFC unaotarajiwa kupigwa majira ya saa moja [19:00] katika uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Jijini Dar Es Salaam.

Yanga imepanga kuutumia mchezo wa leo kama sehemu ya maandalizi kuelekea mchezo wa Ligi ya mabingwa Barani Afrika dhidi ya CR Belouizdad unaotarajiwa kupigwa Jumamosi hii kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa, Jijini Dar Es Salaam.

Kuelekea mchezo huo, hizi ndizo takwimu zinazoonyesha baada ya timu hizi mbili kukutana kwenye michezo mitano ya mwisho;

  • Yanga imeshinda michezo minne [4] kati ya michezo mitano ambayo timu hizi zimekutana na imefunga magoli tisa [9] na imefungwa magoli mawili [2].
  • Polisi Tanzania haijapata ushindi wa aina yoyote katika michezo mitano ya mwisho iliyopita, imetoa sare mchezo mmoja pekee na imefunga magoli mawili [2].
  • Yanga inashiriki Ligi kuu kandanda Tanzania Bara msimu huu huku Polisi Tanzania inashiriki Championship.
  • Klabu ya Polisi Tanzania ipo nafasi ya nane kwenye msimamo wa Ligi ya Championship ikiwa imecheza michezo 22 na imekusanya alama 29.
  • Hadi hivi sasa Polisi Tanzania kwenye ligi imefunga magoli 19 imefungwa magoli 23, imeshinda mechi nane, imepoteza mechi 9 na imetoa sare mechi 5.
  • Yanga inashiriki Ligi kuu kandanda Tanzania Bara, inaongoza msimamo wa Ligi ikicheza michezo 16 na kukusanya alama 43.
  • Yanga imefunga magoli 39 na imefungwa magoli 8, imepoteza mchezo mmoja, imetoa sare mchezo mmoja na imeshinda michezo 14.

Kuelekea mchezo huu wa leo klabu ya Polisi Tanzania imeitaka klabu ya Yanga kujiandaa vyema kwani wao wamejipanga kutoa dozi nene kwa mwananchi.

“Bora wangedeka tu, lakini kwa vile wamekubali wenyewe hawataamini macho yao. Katika kipindi kama hiki tutawatupa rumande mpaka Jumamosi bila dhamana na hatuogopi kutupiwa yale mavitu yao”, Taarifa ya Polisi Tanzania kutoka ukurasa wake wa Instagram.

Baada ya mchezo huu Yanga itashuka dimbani siku ya Jumamosi kuikabili CR Belouizdad kwenye mchezo wa Ligi ya mabingwa Barani Afrika katika uwanja wa Taifa, Jijini Dar Es Salaam.

Popular Posts

Exit mobile version