Mabingwa wa Afrika Al ahly wameomba mechi yao dhidi ya Madeama ichezwe jumamosi badala ya ijumaa baada ya usafiri wao wa ndege kupata hitilafu wakiwa uwanja wa ndege wa Accra International airport na kushindwa kwenda Kumasi ambako mechi inatakiwa kuchezwa huko.
Kwenye maelezo waliyotoa Al ahly kwa CAF wanadai jumatano wakiwa Accra ndege waliyosafiri nayo ilipata hitilafu hivyo hawakupata usafiri mwingine wa kuwafikisha Kumasi kwa wakati.
Licha ya jitihada za kupata ndege mbadala ya ndani, timu ya Al Ahly ililazimika kulala mjini Accra, na hivyo kukwamisha mipango yao ya kuwasili na kufanya maandalizi kwa wakati.
Kwa mujibu wa kanuni za Ligi ya Mabingwa Afrika, Al Ahly wanatakiwa kufanya mazoezi katika uwanja wa mechi siku ya Alhamis.
Kwa kuzingatia itifaki za mashindano, Al Ahly wamewasiliana na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), wakitaka kuahirishwa kwa siku moja kwa mechi iliyopangwa kuchezwa kwenye Uwanja wa Baba Yara siku ya Ijumaa.
Klabu hiyo inasubiri majibu ya CAF ili kukabiliana na changamoto zisizotarajiwa ambazo wajumbe wao walikutana nazo katika safari yao ya kwenda kukabiliana na Medeama.
Al Ahly, Yanga,CR Belouizdad na Medeama zipo kundi moja na kila timu kwenye kundi hili D ina nafasi ya kufuzu robo fainali.