Azam Sports Federation

SIMBA YAIKAMUA TRA KILIMANJARO

Published on

Simba wamefanikiwa kutinga hatua ya 16 bora ya michuano ya Azam Sports Federation Cup baada ya kuitandika timu ya daraja la pili ya TRA Kilimanjaro kwa mabao 6-0 kwenye mchezo uliopigwa kwenye dimba la Azam Complex, Chamazi.

Simba walitengeneza nafasi za mapema na dakika ya 8 tu Ladack Chasambi alipiga shuti nje ya eneo la 18 Lakini golikipa wa TRA aliokoa shuti hilo.

Alikuwa ni Ladack Chasambi aliyeitanguliza Simba dakika ya 12 akitumia makosa ya walinzi wa TRA kushindwa kuokoa mpira uliokuwa ukizengea golini na yeye kupiga kupiga shuti lililotinga golini moja kwa moja.

Ulikuwa ni mchezo wa njia moja kwa muda mwingi japo TRA walijaribu kuzuia mianya mingi ya nafasi zilizokuwa zikitengenezwa na Simba.

Dakika ya 40, Sadio Kanoute alitumia akili kubwa ya faulo ya Mzamiru Yassin na yeye kupiga mkwaju wa chini chini uliomshinda golikipa wa TRA na kuiandikia timu yake bao la 2.

Freddie Kouablan alipata nafasi ya wazi ya kuandika bao la 3 kwa Simba lakini akapiga shuti nje ya lango kabisa akiwa anatazamana tu na golikipa.

Simba walienda mapumziko wakiwa kifua mbele kwa mabao 2-0.

Mazungumzo ya chumba cha kubadilishia nguo kipindi cha mapumziko kiliirudisha Simba ikiwa na moto sana.

Dakika ya 50 kipindi cha pili, Freddie Kouablan alipachika bao la 3 kwa Simba akitumia vema kabisa krosi ya David Kameta Duchu.

Ikaanza kuwa karamu ya magoli kwa Simba, ndani ya dakika 5, walifunga bao la 4 na la 5 yote yakifungwa na Sadio Kanoute.

Dakika ya 53, Sadio Kanoute alitengewa pasi nzuri na Kibu Denis akiwa ndani ya kisanduku na kuachia shuti kali lililomshinda golikipa wa TRA na kuandika bao la 4.

Sadio Kanoute alikamilisha HatTrick yake dakika ya 55 kwa kupachika goli lake la 3 na la 5 kwa Simba akipokea tena kazi nzuri ya Kibu Denis na kumdokolea tu mlinda lango aliyekuwa na hana cha kufanya.

Benchikha alifanya mabadiliko kwa kuwatambulisha mchezoni, Luis Miquissone, Edwin Balua, Pa Omar Jobe na Mohamed Karabaka kuchukua nafasi za Abdallah Hamisi, Kibu Denis, Ladack Chasambi na Freddie Kouablan.

Haikumchukua muda Pa Omar Jobe kuingia kwenye ubao wa magoli, dakika ya 72 aliipatia Simba goli la 6 akitumia vizuri pasi mpenyezo ya Mzamiru Yassin na kudokoa tu mpira kupishana na golikipa Mahmoud Lipangala.

Babacar Saŕr aliingia pia kuchukua nafasi ya Mzamiru Yassin.

Salehe Karabaka alipata nafasi nje ya kisanduku na kuachia mkwaju mkali uliopita nje kidogo ya lango la TRA dakika ya 78.

Simba waliendelea kusukuma mashambulizi na kutengeneza nafasi nyingi za kufunga lakini hazikutumiwa. Mpaka dakika zote 90 zinatamatika, Simba 6-0 TRA.

Popular Posts

Exit mobile version