Nyota wa klabu ya Juventus Paul Pogba amefungiwa kujihusisha na soka kwa miaka minne baada ya uchunguzi kubainika kuwa alikuwa anatumia dawa za kuongeza nguvu.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 30 amesema yupo na mpango wa kukata rufaa kwenye mahakama ya usuluhishi michezoni juu ya hukumu hiyo aliyoipokea.
“Leo nimetaarifiwa kuhusu maamuzi ya TNA [Tribunale Nazionale Antidoping] na naamini uamuzi huo sio sahihi.”
“Nimesikitishwa sana, nimeshtuka na nimeumizwa na kila kitu nilichokitengeneza kwenye maisha yangu ya mpira wa miguu kimeondolewa kwangu.”
“Nikitoka kwenye vizuizi vya kisheria kila kitu kitakuwa wazi, lakini sikuwahi kwa kujua au makusudi kukiuka sheria zinazokataza matumizi ya dawa michezoni.”
“Kama mwanamichezo wa kulipwa siwezi kufanya chochote kuongeza uwezo wangu uwanjani kwa kutumia vitu vilivyozuiliwa, sijawahi kuwakosea au kuwaongopea wanamichezo wenzangu na mashabiki wa timu yoyoye niliyoichezea au niliyocheza dhidi yao.”
“Kutokana na maamuzi yaliyotangazwa leo, nitakata rufaa kwenye mahakama ya usuluhishi michezoni.”
Ameandika Paul Pogba baada ya taarifa kutoka kuwa amefungiwa kujihusisha na soka kwa miaka minne kutokana na matumizi ya dawa zilizokatazwa michezoni.