Boxing

SELEMANI KIDUNDA, ASEMAHLE WELLEM HAKUNA MBABE

Published on

Pambano la Mkanda wa WBF : WORLD BOXING FOUNDATION kati ya Bondia Mtanzania Selemani Kidunda na Asemahle Wellem wa Afrika Kusini Lililofanyika kwenye Ukumbi wa Warehouse, Masaki, Dar Es Salaam, limemalizika kwa SARE. Asemahle akibaki na Mkanda wake.

RAUNDI YA KWANZA

Ilikuwa ni raundi ya mabondia wote kuangaliana uwezo na madhaifu. Huku wakibadilishana ngumi za kudokoana kupimana utimamu.

RAUNDI YA PILI

Selemani Kidunda aliingia raundi hii akiwa na utulivu huku akipiga “Jabs” na “Counterpunch” nyingi. Asemahle Wellem pia hakuwa mnyonge kurusha makonde Lakini Kidunda alikuwa timamu kiuvumilivu na kukwepa kadhaa pia.

RAUNDI YA TATU

Kidunda aliingia na kasi kubwa ya kushambulia, sekunde chache tu ndani ya raundi ya 3, Asemahle alidondoshwa chini kwa mara ya kwanza tangu aanza kucheza ngumi za kulipwa lakini alitumia uzoefu wake kurejesha nguvu na kukwepa ngumi za Kidunda ambaye alitaka kumaliza pambano huku na yeye akirusha makonde kadhaa kwa Kidunda. Raundi ilitamatika kwa Kidunda kutoka akiwa na uvimbe juu ya jicho.

RAUNDI YA NNE

Asemahle aliamua kuchungulia zaidi jicho la kulia la Sele Kidunda ambalo lilionekana kama kuanza kufunga. Hata hivyo haikumzuia Kidunda kurusha ngumi. Haikuwa raundi ya mapigano sana kwani mabondia wote walijaribu kusomana tena baada ya raundi iliyopita kuwa na maseke sana.

RAUNDI YA TANO

Raundi hii ilianza kuonekana kutumika mbinu ya Ngumi za mwilini, Asemahle akirusha na Kidunda akirusha. Mara chache zilikuwa zikitumika “Combination”.

RAUNDI YA SITA

Mchezo ulizidi kushika kasi huku Asemahle akiendelea kutumia zaidi mbinu yake ya Jab ambayo ni ya mkono wa kushoto. Uhodari wa Kidunda ulimuwezesha kumudu ngumi zake, guard yake ilikuwa nzuri sana.

RAUNDI YA SABA

Selemani Kidunda aliichukua raundi hii akifanikiwa kurusha ngumi nyingi ambazo zilimfikia vilivyo Asemahle. Kwa mara nyingine tena alienda chini Asemahle lakini akionekana kuteleza. Raundi ilimalizika Kidunda akiwa na moto zaidi.

RAUNDI YA NANE

Mabondia wote wawili walirudi chini. Asemahle akirusha Jab na kutembea huku Kidunda akirusha ngumi na kutembea. Ikawa ni raundi ya kupoza zaidi kasi ya mpinzani. Uvumilivu ulikuwa ni ufunguo katika raundi hii.

RAUNDI YA TISA

Asemahle aliamua kurudi na kasi raundi hii. Akirusha ngumi mfululizo kujaribu kumchanganya Kidunda. Selemani alikuwa makini sana kumsoma na kumtuliza. Pengine ilikuwa ni raundi ambayo Selemani alikuwa nyuma sana kwa Asemahle ambaye alionekana kuitawala raundi hii.

RAUNDI YA KUMI

Mambo yalianza kuwa ya moto zaidi raundi hii, Asemahle akiendeleza alipoishia. Akiwa na utashi mkubwa wa kukwepa lakini pia akimrushia makonde kadhaa Kidunda yaliyomfikia. Ni raundi ambayo Jab nyingi zilimfikia Selamani, ni utimamu wake na uvumilivu vikamfanya kumaliza raundi hii salama.

RAUNDI YA KUMI NA MOJA

Selemani Kidunda alijibu mapigo raundi hii na kumfanya Asemahle Wellem kukumbatia sana. Lakini zilikuwepo nyakati Selemani pia alikuwa akikumbatia ni kama kila mtu alikuwa anaanza kuchoka. Shughuli ilionekana kuwa nzito.

RAUNDI YA KUMI NA MBILI

Raundi ya umakini zaidi kwa mabondia wote wawili. Kila bondia akiamini kashinda hivyo kulinda alama zake ndicho kilichoonekana zaidi kwenye raundi hii japo mara kadhaa Kidunda alionekana kufikiwa na ngumi za Asemahle mpaka kudondoshwa mara moja. Haikuwa raundi ya ufundi mwingi ila kila bondia alionekana kujilinda muda mwingi, mara chache Kidunda alionekana kuwa “offguard”.

MATOKEO

JAJI NAMBA 1 :114-114

JAJI NAMBA 2 :116-111

JAJI NAMBA 3 : 113-113

Kwa Matokeo Haya Mchezo Ulimalizika kwa SARE.

Mabondia wote wawili walisifiana kiuwezo na wote walikuwa tayari kwa ajili ya Kurudiana wakati wowote.

Popular Posts

Exit mobile version