Yanga wamepoteza nafasi ya kumaliza Vinara wa Kundi B baada ya kukubali kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Al Ahly kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa CAF Uliopigwa kwenye dimba la Cairo International japokuwa timu zote tayari zimefuzu hatua ya Robo Fainali ya michuano hiyo.
Mchezo ulianza kwa kasi ya chini dakika 15 za mwanzo huku Al Ahly wakionekana kufaidi zaidi umiliki wa mpira na Yanga wakicheza kwa nidhamu ya hali ya juu hasa kwenye eneo lao.
Dakika ya 20, Percy Tau alidhani kaipatia timu yake bao la utangulizi akipokea pasi mserereko ya Ali Maloul lakini kibendera tayari kilikuwa juu kuashiria Maloul alikuwa kwenye eneo la kuotea wakati anapokea pasi kabla hajapiga pasi ya usaidzi.
Joseph Guede alipigiwa krosi nzuri na Joyce Lomalisa Mutambala lakini Shuti lake likaenda nje kidogo ya lango.
Dakika ya 42, Pacome Zouzoua aliwachezesha Walinzi wa Al Ahly na akiwa anatizamana tu na golikipa Mustafa Shoubir, alikataliwa shuti lake.
Al Ahly walipata nafasi dakika ya 44 kupata bao kupitia pigo la adhabu nje kidogo ya eneo la 18 Lakini Ali Maloul alipaisha pigo lake.
Timu zote zikionekana kucheza kwa umakini sana hasa kwenye maeneo yao ya kujilinda, iliakisi matokeo ya 0-0 ya kipindi cha kwanza. Licha ya nafasi zilizopatikana, kila timu ilikuwa makini sana kiulinzi huku eneo la pembeni likitumika zaidi.
Kipindi cha pili Al Ahly waliingia na kupata bao la utangulizi mapema tu dakika ya 46, akilianzisha shambulizi yeye mwenyewe Hussein El Shahat, akimpasia Ali Maloul akamrejeshea pasi hiyo El Shahat ambaye alipiga shuti golikipa Djigui Diarra akiwa hayupo langoni na kuiandilia Al Ahly bao la 1. 1-0 Al Ahly.
Yanga walilazimika kufanya utulivu. Dakika ya 50 walipata faulo nje kidogo ya eneo la Al Ahly, krosi nzuri ya Pacome Zouzoua ilitua kichwani mwa Kennedy Musonda lakini mpira wake uliokolewa na golikipa Mustafa Shoubir.
Al Ahly waliendelea kuwasakama Yanga, Djigui Diarra akiwekwa kazini. Dakika ya 59 Anthony Modeste aliunganishwa kwa kichwa krosi nzuri ya Marwan Attia lakini Diarra alikuwa sambamba nalo.
Makocha wote wawili walilazimika kufanya mabadiliko dakika ya 73 kutokana na sababu za majeruhi na kiufundi, Yanga waliwapumzisha Joyce Lomalisa na Khalid Aucho wakiwaingiza Nickson Kibabage na Salum Aboubakar huku Al Ahly wakiwapumzisha Ahmed Kouka, Hussein El Shahat na Anthony Modeste wakiingia Emam Ashour, Taher Mohamed na Wessam Abou Ali.
Al Ahly walifanya tena mabadiliko dakika ya 83 wakimtambulisha mchezoni Reda Slim kuchukua nafasi ya Percy Tau huku Amr El Solaiya akitoka na kuingia Afsha. Yanga nao walifanya mabadiliko hapo hapo akiingia Clement Mzize nafasi ya Kennedy Musonda.
Yanga iliwalazimu kutoka nyuma ili kusogea kujaribu kusawazisha. Lakini nyakati ambazo hawakuwa na mpira waliishi kihatarishi sana kwani Al Ahly walikuwa na wachezaji wengi wenye kasi ndani ya Kiwanja.
Dakika ya 90+1 Yanga walimtambulisha mchezoni Augustine Okrah kuchukua nafasi ya Azizi Ki.
Dakika zote 90 zilitamatika kwa Al Ahly kuibuka na ushindi wa bao 1-0 na kuhakikisha wanamaliza kundi D wakiwa vinara.