Baada ya kipigo cha mabao 4-1 kutoka kwa Azam, Dodoma Jiji wamerejea kwenye njia ya ushindi baada ya kuwafunga Tabora United 1-0 kwenye mchezo wa ligi kuu Tanzania Bara uliopigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma. Matokeo yanayowasogeza hadi nafasi ya 9 wakifikisha alama 23 huku Tabora United wakishuka hadi nafasi ya 12 wakisalia na alama 21.
Nafasi ya wazi ya mapema waliipata Dodoma Jiji kupitia kwa Hassan Mwaterema aliyeunganisha krosi kwa shuti dogodogo lililomshinda golikipa Ibrahim Isihaka lakini alikuwa kwenye mstari Lulihoshi na kuokoa shambulizi hilo.
Dakika ya 28, Alikuwa ni Hassan Mwaterema tena aliyepata nafasi ya kupiga shuti kali lakini golikipa Ibrahim Isihaka alifanya wokovu mara mbili.
Tabora United walienda kuishi hatarini, Faulo nzuri iliyochongwa na Gustapha Simon iliokolewa vema tena na Ibrahim Isihaka.
Kipindi cha kwanza kilimilikiwa vilivyo na Dodoma Jiji kasoro kupata goli tu. Mpaka mapumziko Dodoma Jiji 0-0 Tabora United.
Kipindi cha pili timu zote zilirudi kwa kasi ya kushambulia kupata matokeo, Dodoma Jiji wakimtambulisha Yassin Mgaza mchezoni kuimarisha eneo lao la Ushambuliaji.
Huku Tabora United wakiboresha eneo la kiungo kwa kumtoa Emotan Cletous ambaye hajawa na wakati mzuri hii leo na nafasi yake kuchukuliwa na Najim Mussa. Dodoma Jiji wakimuongeza pia Paul Peter Kasunda nafasi ya Zidane Sereri.
Dakika ya 71, Daniel William Lukandamila alipata nafasi nje kidogo ya eneo la 18 na kuachia mkwaju uliopanguliwa na golikipa Mohamed Hussein wa Dodoma Jiji. Bado milango ikaendelea kuwa migumu.
John Ben Nakibinge alipata nafasi pia dakika ya 75 akitumia mpira ambao haukuokolewa vizuri na walinzi wa Dodoma Jiji lakini mpira wake uliokolewa kwenye mstari na Anderson Kimweri.
Dodoma Jiji walijibu mapigo kupitia kwa Paul Peter Kasunda aliyepiga shuti nje ya eneo la penati la Tabora United lakini Ibrahim Isihaka alipangua vizuri shuti hilo.
Dakika ya 77, Apolo Otieno alipata nafasi ya kupiga shuti la mbali lakini kwa mara nyingine tena Ibrahim Isihaka alisimama imara.
Iddy Kipagwile aliyechukua nafasi ya Meshack Abraham alipiga mpira wa pigo huru kwa ustadi mkubwa kabisa lakini Ibrahim Isihaka aliyekuwa na siku nzuri leo, akaokoa na kona iliyotokana haikuwa na madhara.
Wakati huo Tabora United walimuinigiza Athuman Abasa nafasi ya Banza Kalumba.
Krosi ya Peter Peter Kasunda dakika ya 90+1 ilishindwa kuokolewa vizuri na walinzi wa Tabora United na mpira uliombabatiza mlinzi Shaffih Maulid ukamdondokea Hassan Mwaterema aliyejisogezea tu na kuachia shuti la chini chini safari hii likimshinda Ibrahim Isihaka. Goli la ushindi kwa Dodoma Jiji.
Dakika zote 90 zikatamatika kwa Dodoma Jiji kuibuka na ushindi wa bao 1-0.