CAF Champions League

AHMED ALLY: TUNAENDA KUFUZU NUSU FAINALI CAF CL.

Published on

Klabu ya Simba imeanza kufanya hamasa kwa mashabiki zake kuelekea mchezo wa robo fainali ya Ligi ya mabingwa Barani Afrika dhidi ya Al Ahly.

Mchezo huo wa kwanza utapigwa katika dimba la Benjamin Mkapa, Ijumaa ya March 29 majira ya saa tatu [21:00] usiku kwa saa za Afrika Mashariki.

Wakati wa ufunguzi wa hamasa hizo, Afisa habari na mawasiliano wa klabu ya Simba Ahmed Ally ametanabaisha kuwa klabu yao imechoka kuishia robo fainali na sasa wanaitaka nusu fainali.

“Tunakwenda kucheza mechi dhidi ya Al Ahly, lazima tuelezane ukweli kwamba hii ni mechi ngumu kweli kweli. Hii inakuwa robo fainali yetu ya tano mfululizo ya michuano ya CAF. Kwanza kama taasisi lazima tujivunie muendelezo wetu wa matokeo mazuri ndio maana tumefanikiwa kucheza robo fainali tano mfululizo.”

“Sasa tumechoka robo fainali, tunataka nusu fainali. Hii ni zamu yetu kwenda nusu fainali. Iwe jua iwe mvua, iwe Ramadhani iwe Kwaresma tunaitaka nusu fainali, hakuna mjadala mwingine.”

“Hatuna option nyingine safari hii, option ni moja tu tunaitaka nusu fainali. Na hii ndio salamu yetu Wanasimba wiki hii, ukikutana na Mwanasimba mwenzako mwambie Tunaitaka Nusu Fainali. Slogan ni Tunaitaka Nusu Fainali. Tumeshaanguka sana sasa ni muda wetu kusimama.”- Ahmed Ally.

Licha ya mambo mengi aliyozungumza kuelekea mchezo huo Ahmed Ally akaweka wazi viingilio vya mchezo huo unaotazamiwa kuwa mkubwa zaidi Barani Afrika kwasasa.

“Viingilio vya mchezo ni;
Mzunguko – Tsh. 5,000
Machungwa – Tsh. 10,000
VIP C – Tsh. 20,000
VIP B – Tsh. 30,000
VIP A – Tsh. 40,000
Platinum – Tsh. 200,000
Tanzanite – Tsh. 250,000
Tunaamini viingilio hivi ni rafiki kwa kila Mwanasimba.” – alisema Ahmed.

Klabu ya simba kwasasa imekita kambi visiwani Zanzibar na inatarajiwa kucheza michezo miwili ya kirafiki ikiwa huko, mmoja dhidi ya al hilal ya Sudan na nyingine dhidi ya JKU ya Zanzibar.

Popular Posts

Exit mobile version