CAF Champions League

KUKOSEKANA KWA AUCHO, PACOME KULIIBADILISHA YANGA JANA.

Published on

Klabu ya Yanga imetoka sare ya bila kufungana na Mamelodi sundowns kwenye mchezo wa kwanza wa robo fainali wa Ligi ya mabingwa Barani Afrika uliopigwa katika dimba la Benjamin Mkapa, Jijini Dar Es Salaam.

Hii inakuwa mara ya pili kwa timu hizi mbili kutoka sare kwenye michezo ya Ligi ya mabingwa baada ya mara ya kwanza kutoa sare ya 3-3 katika uwanja wa CCM Kirumba, Jijini Mwanza.

Yanga kwenye mchezo wa jana walicheza kwa tahadhali kubwa kutokana na ubora wa mpinzani wake Mamelodi Sundowns, Kocha mkuu wa Yanga Miguel Gamondi akianza na mabeki watano, viungo watatu na washambuliaji watatu [4-3-3].

Gamondi alianza kwa mfumo wa kujilinda zaidi kutokana na ubora wa safu ya ushambuliaji ya Mamelodi Sundowns lakini pia kukosekana kwa baadhi ya nyota wake muhimu kwa wakati mwingine kilisababisha kuanza kwa tahadhali kubwa.

Yanga ilipata nafasi kadhaa kwenye mchezo wa jana lakini washambuliaji wake Kennedy Musonda, Clement Mzize na Stephen Aziz Ki walikosa utulivu wa kuzimalizia nafasi hizo lakini pia ubora wa golikipa Ronwen Williams wa Mamelodi Sundowns uliwanyima nafasi ya kuiandikia Yanga goli.

Bakari Nindo Mwamnyeto, Dickson Job na Ibrahim Hamad walikuwa na kiwango bora sana kwenye eneo la ulinzi wakisaidiwa na Jonas Mkude ambaye kwa mara ya kwanza alionekana kuanza jana.

Yanga iliwakosa baadhi ya nyota wake mhimu hapo jana ikiwemo Khalid Aucho, Pacome Zouzoua na Yao Kouassi Attohoula ambao wote bado hawajaimarika baada ya kupata majeraha.

Mchezo wa marejeano kati ya klabu hizi mbili unatarajiwa kufanyika kwenye dimba la Loftus Versfield, Jijini Pretoria nchini Afrika Kusini mwishoni mwa wiki Ijayo.

Kuelekea mchezo huo huenda Yanga ikawatumia nyota wake Yao Kouassi, Pacome Zouzoua na Khalid Aucho ambao wameanza mazoezi na kikosi kingine.

Popular Posts

Exit mobile version