CAF Champions League

SIMBA NA YANGA MATUMAINI KIBAO UGENINI CAF

Published on

Timu za Simba na Yanga zimeshaondoka nchini kuelekea Misri na Afrika Kusini kwa ajili ya mechi zao za mkondo wa pili hatua ya Robo Fainali ya Michuano ya Ligi Mabingwa Afrika.

Yanga waliondoka mapema jana kuelekea Pretoria kuwakabili wenyeji wao Mamelodi Sundowns ambao wao walikuwa na Mchezo jana wa ligi kuu wakishinda 1-0 dhidi ya Richards Bay huku wakiwa na kumbukumbu ya kutoka suluhu ya 0-0 jijini Dar es Salaam.

Simba wao wameondoka alfajiri ya kuamkia leo kuelekea Cairo kuwakabili Al Ahly ambapo kwenye mchezo wa kwanza Simba alikubali kufungwa bao 1-0 nyumbani, goli la Ahmed Kouka likiweka ugumu kwenye nafasi ya Simba kufuzu hatua hii.

Licha ya matokeo ya awali ya kutopata ushindi nyumbani, bado timu zote zimeondoka na matumaini kibao kuelekea michezo hii huku kila timu ikiamini kwenye kutimiza malengo yao ikiwemo kufuzu nusu fainali.

Makocha wote wameonyesha nia ya kuendea michezo hii kwa tahadhari kubwa lakini wakiwa na imani pia kwa vikosi vyao kuwa vinaweza kufanya makubwa ugenini.

Kocha wa Simba Abdelhak Benchikha anaamini kuwa hawana cha kupoteza watapoenda Misri bali ni kupambana kwa kila hali na kuwafanya Al Ahly ndio wawe na presha na mchezo akiamini pia kuwa kupata bao la mapema na kuweka mzani sawa utauchangamsha zaidi mchezo.

Upande wa Yanga kurejea kwa wachezaji wao nyota hasa Pacome Zouzoua kunaibua matumaini zaidi kuelekea mchezo huo huku Kocha wa Yanga Miguel Gamondi naye akionyesha kuwa hana hofu na kikosi chake na anaamini watafanya vizuri.

Kila la Kheri kwa timu zetu zote hizi kwenye Uwakilishi huko Bondeni na Cairo. Tunaamini kwenye uwezo wenu na mtaliheshimisha taifa.

Popular Posts

Exit mobile version