NBC Premier League

COASTAL UNION YATAKATA LAKE TANGANYIKA

Published on

Coastal Union wameendelea kuonyesha dhamira yao ya kucheza soka la Kimataifa msimu ujao baada ya kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mashujaa kwenye dimba la Lake Tanganyika, Kigoma wakikita mizizi kwenye nafasi ya 4.

Mangush walitangulia dakika ya 10 tu ya mchezo kwa goli maridadi kabisa la Shadrack Mulungwe ambaye alilianzisha mwenyewe wakigongeana vizuri na Jackson Katanga Shiga aliyemnyunyizia krosi na yeye kuunganisha kwa kichwa.

Mchezo ukaendelea kushika kasi kwa timu zote mbili kufunguka huku Mashujaa wakionyesha ari ya kutaka kusawazisha lakini Coastal Union walikuwa imara.

Coastal Union walidhani wamepata bao la 2 dakika ya 12 lakini kibendera kilikuwa juu kuashiria Daudi Semfuko alikuwa kwenye nafasi ya kuotea wakati anafunga.

Ikiwa imesalia dakika 1 tu kuelekea mapumziko, Omari Omari alijitengenezea nafasi mwenyewe na kuachia shuti kali lililomshinda golikipa wa Coastal Union Chuma Ramadhani na kuisawazishia timu yake kubadili mazungumzo kwenye vyumba vya kubadili nguo.

Timu zote zilirejea kwa kasi kipindi cha pili wakijaribu kutafuta bao la mapema na pengine la ushindi.

Dakika ya 58 ya mchezo, wakitumia vizuri mpira wa adhabu kugongeana pasi na pasi ya mwisho ya usaidizi kutoka kwa Shadrack Mulungwa ikamfikia Selemani Bakari akiwa analitazama tu lango la Mashujaa na kukwamisha mpira wavuni kuipa timu yake ya Coastal Union uongozi kwa mara ya pili. 1-2 kwa Coastal Union.

Mashujaa bado walionyesha kuwa mchezoni licha ya kwamba hawakuwa na kasi sana hasa kwenye eneo la kushambulia wakimtegemea Adam Adam ambaye hakuwa kwenye kiwango bora hii Leo.

Coastal Union waliendelea kuushikilia uongozi mpaka dakika ya mwisho ya mchezo na kuhakikisha wanaendelea kujikita kwenye nafasi yao ya 4 wakifikisha alama 33 huku Mashujaa wakibaki nafasi ya 12 wakiwa na alama 21 wote wakiwa wamecheza mechi 22.

Popular Posts

Exit mobile version