African Football League

SIMBA IPO TAYARI KUIVAA AL AHLY KESHO.

Wachezaji wa Klabu ya Simba kupitia kwa nyota wake Willy Onana wamesema kesho wapo tayari kupambana ili warudi na ushindi nyumbani.

Published on

Klabu ya Simba inaendelea na maandalizi yake kuelekea mchezo wa marejeano wa michuano ya African Football League dhidi ya Al Ahly mchezo ambao utapigwa kesho hapa Cairo, Misri. Kocha mkuu wa kikosi cha Simba Robert Oliviera amesema kikosi chake kipo tayari kupambana dhidi ya Al Ahly na wapo tayari kuonyesha uwezo wao wote kesho.

Ni mechi muhimu sana kwetu, lazima tujiandae vizuri na kuonyesha uwezo wetu. Tutawapa wachezaji wetu wote nafasi ya kushiriki. Tunawaheshimu sana Al Ahly na tuna uhakika kuwa Al Ahly watatuheshimu pia kutokana na kiwango tulichokionyesha kwenye mchezo wa kwanza tukiwa kwenye uwanja wetu wa nyumbani. Kwa kuiongelea timu yangu ni miongoni mwa timu saba (7) bora Africa ambazo zinashiriki mashindano haya.

Kocha mkuu wa Simba Robert Oliviera akizungumza na waandishi wa habari.

Wachezaji wa Simba kupitia kwa nyota wa Willy Essomba Onana wamewaahidi mashabiki wao kuwa watapambana katika mchezo huo na watahakikisha wanarejea na ushindi nyumbani.

Uwepo wa mashabiki wengi uwanjani kesho ni kitu ambacho tumekizoea, sio kitu kipya kwetu. Tumekuja hapa tukijua kwamba watakuwa na faida ya uwepo wa mashabiki wao uwanjani, kama ambavyo kocha amezungumza tutapambana tuwezavyo na kuhakikisha tunarudi na ushindi.

Mchezaji wa Simba Willy Onana akizungumza na wanahabari leo hapa Misri.

Mchezo wa kwanza wa African Football League kati ya Simba na Al Ahly ulimalizika kwa sare ya kufungana goli 2-2 katika dimba la Benjamin mkapa, Jijini Dar Es Salaam. Leo Simba inahitaji kupata ushindi wa aina yoyote ile ili iweze kufuzu kwenda hatua ya nusu fainali ya michuano hii.

Popular Posts

Exit mobile version