Klabu ya Simba hii leo imeendeleza wimbi la ushindi katika michezo ya Ligi kuu kandanda Tanzania Bara baada ya kuibuka na ushindi wa goli 2-1 hii leo dhidi ya Ihefu katika dimba la Benjamin Mkapa, Jijini Dar Es Salaam.
Magoli ya Simba yamewekwa kambani na Jean Baleke aliyeipatia timu yake goli la mapema dakika ya 12 ya mchezo baada ya makosa ya Sweetberth Mahundi aliyoyafanya wakati akirudisha mpira nyuma na Jean Baleke akaunasa mpira ule na kupiga shuti kali lililomshinda mlinda lango wa Ihefu Fikirini Bakari na kujaa ndani ya kamba.
Dakika ya 25 ya mchezo Mgunda aliiandikia goli la kusawazisha klabu yake ya Ihefu baada ya golikipa wa Simba Ally Salim kuutema mpira uliopigwa na Mahundi kisha kumkuta Mgunda aliyemalizia mpira ule kiulaini tu akiwa ndani ya eneo la 18.
Kipindi cha pili cha mchezo Simba waliandika bao la ushindi dakika ya 25 kupitia kwa Moses Phiri aliyeingia kuchukua nafasi ya Jean Baleke baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa Luis Miquissone.
Simba sasa anafikisha alama 18 akiwa nafasi ya pili (2) katika msimamo wa Ligi nyuma ya vinara Yanga, inasalia kubaki timu pekee ambayo haijapoteza mchezo wowote ndani ya Ligi kuu kandanda Tanzania Bara.
Tangu msimu huu ulipoanza Simba imecheza michezo kumi na mbili (12) kwenye mashindano yote na haijapoteza hata mmoja.