Azam FC wamepata ushindi wa pili ugenini baada ya kuwafunga Ihefu 3-1 kwenye mchezo wa ligi kuu ya NBC uliopigwa kwenye uwanja wa Highland Estates ushindi uliowafanya wakwee kileleni mwa msimamo wakiwa na alama 19 baada ya michezo 9.
Azam FC waliingia wakiwa na mbadiliko makubwa ya kimfumo kwenye kikosi chao, pengine wakiiheshimu Ihefu ugenini. Pakionekana wakiwa na umbo la walinzi wengi la 3-4-3, walinzi watatu wa kati, huku kwenye kiungo pakiwa na mabeki wa pembeni wawili na viungo wakabaji wawili katikati, washambuliaji watatu juu. Walionekana kuwamudu kwa kiasi kiubwa Ihefu kwani timu nzima ilikuwa inakaba tena kuanzia juu, haikuwa rahisi kwao kutengeneza nafasi waliokuwa na mfumo wa 4-2-3-1.
Dakika ya 26 ya mchezo, Never Tigere alipiga vizuri mpira wa adhabu kubwa kwa ubora wa hali ya juu lakini golikipa Ahamada alikuwa sambamba na pigo hilo.
Dakika ya 33, Sospeter Bajana alitumia nafasi ya mpira uliokuwa unazagaa kutokana na kipa Fikirini Bakari kuokoa shuti la Kipre Jr. na shuti lake likaokolewa vizuri na Fikirini.
Dakika ya 34, Feisal Salum akaiandikia bao timu yake akiunganisha kona iliyotokana na shambulizi hilo ya Paschal Msindo kwa kichwa maridadi sana akifunga bao lake la 5 msimu huu.
Azam bado walionekana wapo mbele kwenye kila kitu kwenye mchezo huu, wakitengeneza nafasi nyingi lakini bado hawakuweza kuongeza goli la pili na kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa bao 1-0.
Ihefu waliingia kipindi cha pili na kuamua kuua mfumo wa 4-2-3-1 na kurudi kwenye 4-4-2, akiingia mshambuliaji Jafary Kibaya kuungana na Ismail Mgunda kwenye safu ya ushambuliaji na kummpunguza kiungo mmoja mkabaji, Geofrey Manyasi.
Ni kama walijianika kwenye eneo la kiungo, na Azam waliwaadhibu mapema tu kwenye dakika ya 46 ya mchezo, dakika ya 1 tu ya kipindi cha pili kwa goli la Sospeter Bajana akimalizia kwa shuti kali la chini baada ya Sillah kushindwa kumalizia vizuri krosi ya Nathaniel Chilambo, na yeye kukutana nao na kufunga upande wa kulia wa Fikirini. 2-0 Azam.
Haikuwa Sinema, Sospeter Bajana akawatandika tena Ihefu dakika ya 47 ya mchezo. Paschal Msindo alikimbia na mpira kaktikati ya uwanja na kupiga pasi nzuri pembeni kwa Kipre Jr, aliyepiga pasi nzuri katikati kama pasi ya V ilyommkuta mfungaji ambaye hakufanya ajizi. 3-0 Azam.
Ihefu walitaka kurejea mchezoni lakini ni kama kufuli walilofunga Azam ufunguo umepotea. Walikuwa haraka sana kwenye kufanya majukumu yote mawili, kushambulia na kukaba tena wakiwa kwenye namba nyingi. Ingehitajika kazi ya ziada sana kulibadili hili, lakini kutoka kwa Manyasi kulikifanya kiungo chao kuwa wazi sana. Azam walifanya walichotaka.
Rajabu Athumani, Nassor Saadun na John Kitenga waliingia kuchukua nafasi za Rashid Juma, Never Tigere na Joseph Mahundi kuimarisha safu yao ya Ushambuliaji kuangalia kama watapata chochote huku Azam na wakiwapumzisha Gibrill Sillah na Pascal Msindo na Kumuingiza Abdul Sopu na Cheikh Sidibe.
Azam walipunguza kasi dakika za mwisho za mchezo hali iliyowaruhusu Ihefu kujiamini kutafuta nafasi ya goli, dakika ya 90 ya mchezo, Jafary Kibaya aliifungia bao la kufuta machozi Ihefu na mchezo kumalizika 1-3, Azam wakiwa washindi.