Yanga

WANANCHI WAJITOKEZA KUNYWA SUPU.

Published on

Mashabiki na wadau wa soka mbalimbali katika viunga vya Jiji la Dar Es Salaam leo wamejitokeza kwa wingi katika viwanja vya Jangwani yalipo makao makuu ya klabu ya Young Africans kwaajili ya kunywa supu, licha ya kuwa na hali ya mvua katika Jiji la Dar Es Salaam.

Young Africans walitangaza zoezi la unywaji wa supu baada ya kupata ng’ombe watano kutoka kwa katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Paul Christian Makonda ikiwa ni sehemu ya ahadi aliyoitoa kwa timu itakayoshinda kwenye mchezo wa Derby ya Kariakoo atapatiwa ng’ombe kulingana na idadi ya magoli aliyofunga.

Young Africans iliifunga Simba SC magoli 5-1 ugenini katika mchezo wa Ligi kuu kandanda Tanzania Bara iliopigwa katika dimba la Benjamin Mkapa, hii ni mara ya kwanza kwa klabu hii kusherehekea ushindi wa mchezo wa Ligi kwa kunywa supu na mashabiki wake.

Zoezi hili limehudhuriwa na watu mbalimbali sio mashabiki wa Young Africans pekee bali hata mashabiki wa klabu zingine walikuwepo pia. Meneja habari na mawasiliano wa klabu ya Young Africans Ally Shaban Kamwe amewapongeza wote waliojitokeza kwaajili ya zoezi hilo licha ya kuwa na hali ya mvua.

Tulimfunga mtu goli tano kwenye mvua na leo tunakunywa supu kwenye mvua, mvua ina raha yake.

Kwanza niwapongeze sana wanachama na mashabiki wa Young Africans ambao wameitikia kwa wingi kuja hapa, tumelala na mvua, tumeamka na mvua lakini watu hawa wameonyesha kwamba Yanga ni kitu chenye thamani kwenye maisha yao.

Rais wetu wa Young Africans Eng. Hersi Said baada ya kumpa taarifa jana Rais wa FIFA kilichotokea Jumapili iliyopita, amenunua chapati Elfu tano, kwaajili ya wanachama na mashabiki.

Ally Kamwe, Afisa habari na mawasiliano wa klabu ya Young Africans.

Mashabiki wa klabu ya Yanga waliojitokeza pia nao walipata nafasi ya kuzungumza nama hali ilivyo hii leo na walivyolipokea jambo la kunywa supu.

Tumezoea kwenye mvua kwasababu siku tunamfunga mtani ilikuwepo mvua, hizo sio shida zetu, shida zao wenyewe. Tuna waomba tena mchezo ujao wajilegeze tuwapige kumi tuje tunywe tena.

Shabiki mmoja wa Young Africans alizungumza.

Tuna mshukuru mwenyezi Mungu mpaka leo tunafika hapa, nimekula supu na vipande vya nyama vitano, chapati tano.

Tunamshukuru sana Eng. mwenyezi Mungu azidi kumuweka tupate mambo kama haya.

Shabiki mwingine wa Young Africans alizungumza.

Palipo na mashabiki wa klabu ya Young Africans hapakosekani uwepo wa mashabiki wa klabu ya Simba, nao walijitokeza kushiriki katika hafla hiyo.

Nawaona japo inaniumiza lakini asiyekubali kushindwa si mshindani, nimekubali nimeshindwa, nimekuja kunywa supu jamani nipeni supu ya kutosha na mimi nifaidike.

Nashukuru sana kwa ukarimu mliouonyesha watani zangu, nawashauri waendelee kukaza buti, maisha yaendelee

Shabiki aliyevalia jezi ya Simba na kupewa chapati tano.

Leo ilikuwa ni furaha kubwa kwa mashabiki wa klabu ya Young Africans ambao walijumuika pamoja kunywa supu licha ya kuwa na hali ya hewa isiyo rafiki baada ya mvua kuendelea kunyesha katika Jiji la Dar Es Salaam.

Popular Posts

Exit mobile version