Manchester United imepata Ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Everton kwenye mchezo wa ligi kuu ya Uingereza, mechi iliyopigwa kwenye uwanja wa Goodison Park ikishuhudia pengine goli bora la wikiendi hii. Huku ishuhudia kiwango bora sana cha kijana Kobbie Mainoo.
Alejandro Garnacho alifungua akaunti ya mabao kwa United akifunga goli kwa mtindo wa sarakasi/mkasi akiunganisha krosi nzuri ya Diogo Dalot dakika ya 3 tu ya mchezo.
Goli la Garnacho ni kama lilifanya United kujiamini zaidi na kutandaza soka safi dhidi ya wapinzani wao huku wakitengeneza nafasi lukuki lakini walishindwa kuzitumia. Hata hivyo Everton hawakuacha kujibu mapigo kwani ililazimika Andre Onana kufanya kazi ya ziada akiokoa michomo kadhaa ya Calvert Lewin na Idrisa Gana Gueye kwa nyakati tofauti. Mpaka mapumziko, United walikuwa wakiongoza 1-0.
Kipindi cha pili kilirejea na United kuendeleza walipoishia kipindi cha wakiwasukuma Everton golini kwao. Dakika ya 56 ya mchezo United walipata bao la pili kupitia mkwaju wa Penati uliotokana na mshambuliaji Anthony Martial kufanyiwa madhambi kwenye eneo la penati na Ashley Young. Penati hiyo ilifungwa na Marcus Rashford.
United walipata goli la 3 dakika ya 75 ya mchezo kupitia kwa Anthony Martial akimalizia vizuri kazi nzuri aliyoianzisha mwenyewe kabla ya kupokea pasi tamu kutoka kwa Bruno Fernandes na kumalizia kiustadi sana.
Mpaka dakika ya 90 inamalizika, United walifanikiwa kupata alama 3 Muhimu zilizowasogeza Mpaka nafasi ya 6 wakifikisha alama 24, alama 6 tu nyuma ya vinara wa ligi hiyo, Arsenal.