NBC Premier League

KAZADI AFUNGA GOLI LA KWANZA NPL SINGIDA FG.

Published on

Ligi kuu kandanda Tanzania Bara imeendelea hii leo kwa michezo miwili kuchezwa katika viwanja tofauti nchini.

Mkoani Singida katika uwanja wa CCM Liti ulishuhudiwa mchezo kati ya Singida Fountain Gate dhidi ya JKT Tanzania, mchezo ambao ulimalizika kwa sare ya goli 2-2.

Magoli ya Singida Fountain Gate yalifungwa na Marouf Tchakei dakika ya 62 na Francy Kazadi dakika ya 75. Hili ni goli la kwanza kwa Kazadi kuifungia klabu ya Singida katika michezo ya Ligi kuu kandanda Tanzania Bara tangu aliposajiliwa na kikosi hicho kwenye dirisha dogo la usajili la mwezi January msimu uliopita.

Magoli ya JKT Tanzania yalifungwa na Hassan Kapalata dakika ya 26 na Hassan Nassor Maulid dakika ya 68 ya mchezo.

Baada ya mchezo huo Singida Fountain Gate inafikisha alama 19 ikiwa imecheza michezo 12 ikiawa nafasi ya nne [4] ya msimamo na JKT Tanzania ikifikisha alama 16 katika michezo 12 iliyocheza msimu huu na ipo nafasi ya sita [6] ya msimamo.

Mchezo mwingine ulipigwa katika uwanja wa Ali Hassan Mwinyi Mkoani Tabora ambapo mwenyeji Tabora United iliibuka na ushindi wa goli 2-1 dhidi ya Mtibwa Sugar.

Magoli ya Tabora United yaliwekwa kimiani na Eric Okutu dakika ya 19 ya mchezo huku goli la pili kwa upande wa Tabora United likifungwa na Ben Nakibinge dakika ya 32 ya mchezo huo.

Mtibwa Sugar ilipata goli la kufutia machozi katika mchezo huo dakika ya 75 lililofungwa na Kassim Haruna.

Baada ya mchezo huo Tabora United inafikisha alama 14 katika michezo 10 iliyocheza na inapanda hadi nafasi ya nane ya msimamo wa Ligi kuu Kandanda Tanzania Bara.

Mtibwa Sugar ikisalia mkiani mwa msimamo wa Ligi [Nafasi ya 16] ikiwa na alama tano [5] katika michezo 11 waliyocheza hadi hivi sasa.

Kesho Ligi kuu kandanda Tanzania Bara inatarajiwa kuendelea kwa mchezo mmoja kwa kuwakutanisha wakusanya mapato wa manispaa ya kinondoni [KMC] dhidi ya Mashujaa kutoka Kigoma.

Mchezo huo utapigwa majira ya saa 10:00 Jioni katika uwanja wa Uhuru, Jijini Dar Es Salaam.

Popular Posts

Exit mobile version