Timu ya soka ya Mashujaa imeshindwa kupata ushindi nyumbani kwake Lake Tanganyika baada ya muda mrefu kupita wakiambulia sare ya 1-1 dhidi ya Tabora United kwenye mchezo wa ligi kuu soka Tanzania bara.
Itakumbukwa Mashujaa wamefungwa kwenye michezo mitatu mfululizo dhidi ya Azam(0-3), dhidi ya Singida FG(1-3) na dhidi ya KMC(3-2) kabla ya sare ya leo dhidibya Tabora United.
Mashujaa walionekana kuwa na dhamira ya dhati ya kutaka ushindi kwenye mchezo wa leo nyumbani ili kurejesha imani kwa mashabiki wao wakiwa katik kipindi hiki ambacho hawafanyi vizuri sana na dakika ya 12 tu ya mchezo walipata goli la kutangulia kupitia kwa Josephat Jermanus bao lililodumu mpaka mapumziko.
Dakika ya 47 yani dakika ya 2 tu tangu kuanza kipindi cha pili, Tabora United walirejea na nguvu na kufanikiwa kusawazisha bao kupitia kwa Eric Okutu akimalizia pasi yavusaidizi ya Mkongo Jackson Mbombo na kufanya matokeo kusoma 1-1
Mpira ulionekana kushika kasi hasa kipindi hichi cha pili huku pakiwa na mashambulizi ya kujibizana kwa timu zote mbili ambazo zimepanda daraja msimu huu kuonyesha uchu wa kutaka kuondoka na alama zote 3 huku Mashujaa wakionekana kusukuma mashambulizi zaidi lakini walikosa utulivu eneo la kumalizia.
Mpaka dakika ya 90 matokeo yalibaki kuwa 1-1, Tabora United wakiongeza alama 1 na kusogea hadi nafasi ya 8 huku Mashujaa wakiendelea kubaki nafasi ya 15 wakiwa na alama 9 pekee baada ya michezo 10 huku wakiendelea kusubiri ushindi kwa zaidi ya Mwezi sasa.