NBC Premier League

AZAM FC WAENDELEZA DOZI

Published on

Azam FC wamepata ushindi wao wa 4 mfululizo na kukwea kileleni mwa msimamo wa Ligi kuu Tanzania bara baada ya kuwanyuka KMC mabao 5-0 na kufikisha alama 25 baada ya michezo 11 kwenye mchezo uliochezwa kwenye dimba la Azam Complex, Chamazi.

Azam walionyesha kasi ya mchezo kwa kuwapelekea mashambulizi mfululizo KMC ambao walianza mchezo wakiwa chini sana. Baada ya mashambulizi kadhaa kuokolewa na Wilbol Maseke, dakika ya 24 ya mchezo Sospeter Bajana alipora mpira na kumpa pasi Kipre Jr aliyetoa pasi tamu usaidizi kwa Prince Dube aliyepiga mpira kwa mtindo wa mzungusho na kummshinda golikipa Maseke na kuipatia timu yake ya Azam bao la kuongoza.

KMC walijibu haraka baada ya kufungwa kwa kufanya shambulizi la kushtukiza na almanusura wapate bao la kusawazisha dakika ya 25 tu lakini uhodari wa Ahmada ukawaweka Azam salama.

Dakika ya 43, Azam walipata bao la pili baada ya Ismail Gambo kujifunga akiwa kwenye jitihada za kuokoa mpira uliopigwa na Kipre Jr aliyefanya kazi kubwa kuwapunguza walinzi wa KMC.

Mapumziko Azam wanatoka kifua mbele wakiwa na uongozi wa mabao 2-0.

KMC walirudi kipindi cha pili kwa mpango wenye lengo la kutaka kurudisha magoli lakini ni kama lilikuwa kosa kubwa, Azam FC walikuwa bado wana moto wao wa kipindi cha kwanza na dakika ya 51 tu, Prince Dube alifunga bao lake la pili na la 3 kwa Azam.

Wakiwa wanajiuliza wamepigwa na nini, dakika 2 baadae, Gybril Sillah aliandikia Azam FC bao la 4 na kuzidi kuwaweka kwenye wakati mgumu KMC wasijue cha kufanya.

Kosa kubwa la KMC mpaka wakati huo lilikuwa ni kuwaruhusu Azam wacheze wanavyotaka wao yani pembeni mwa uwanja. Boniface Maganga alionekana hamuwezi kabisa Kipre Jr na kwa asilimia kubwa ya mashambulizi yalipitia huko. Pengine KMC wangelitambua hilo mapema wangefanya mabadiliko haraka eneo hilo lakini pia kuwalazimisha Azam wacheze katikati.

Kuendelea kufanya makosa hayo yaliendelea kuiadhibu KMC, dakika ya 60 Feisal Salum alitumia uzembe wa mabeki kushindwa kuuokoa mpira uliokuwa unazagaazagaa golini kwao na kumalizia kiupesi tu kuiandikia Azam bao la 5.

Azam ni kama walidhirika na matokeo na kuamua kuoumzisha silaha zake, Sillah, Dube na Kipre Jr na kuwaingiza Iddy Nado, Aliassane na Sopu. Muda huo ambao KMC wakakumbuka kufunga mlango wao kwa kumuongeza Andre Vincent eneo la Ulinzi.

Mpaka dakika 90 za mchezo zinatamatika, Azam wanapata ushindi wa mabao 5-0 kwa mara ya pili mfululizo kwenye uwanja wao wa nyumbani.

Popular Posts

Exit mobile version