NBC Premier League

PRISONS NA IHEFU ZATAKATA NBC PL

Published on

Ihefu wamefanikiwa kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Tabora United kwenye mchezo wa ligi kuu soka Tanzania bara ikiwa ni ushindi wake wa kwanza baada ya takribani mechi 8 kupita tangu wapate ushindi wa 2-1 nyumbani dhidi ya Yanga.

Ihefu walitangulia kupata bao dakika ya 40 kupitia kwa Vedastus Mwihambi akimalizia kazi nzuri ya Joseph Mahundi.

Dakika ya 56, Vedastus Mwihambi tena aliipatia Ihefu goli la pili na kuifanya Ihefu itanue wigo wa uongozi huku pia wakicheza vizuri mbele ya mashabiki wao kwenye dimba la Highland Estates.

Tabora United walipata bao la kufutia machozi kupitia kwa Andy Bikoko dakika ya 84.

Kwa matokeo haya Ihefu wamesogea mpaka nafasi ya 13 wakifikisha alama 13 baada ya michezo 13. Tabora United wanaendelea kusalia nafasi yao ya 9 wakiwa na alama 15.

Kwingineko kwenye dimba la Lake Tanganyika mkoani Kigoma, zimwi la matokeo mabaya limeendelea kuiandama Mashujaa baada ya kukubali kichapo cha mabao 2-0 nyumbani kutoka kwa Tanzania Prisons.

Tanzania Prisons walipata bao la utangulizi kupitia kwa Jumanne Elfadhil dakika ya 70 akipokea pasi ya usaidizi kutoka kwa Edwin Balua.

Dakika 90+6, Jeremiah Juma alihakikisha wanaondoka na alama zote 3 baada ya kuifungia timi yake bao la pili na kufanya ubao usomeke Mashujaa 0-2 Tanzania Prisons mpaka dakika ya 90.

Prisons wanapanda mpaka nafasi ya 10 wakifikisha alama 14 baada ya michezo 13 huku Mashujaa wakisalia nafasi ya 15 wakiwa na alama zao 9.

Ligi kuu Tanzania bara inatarajiwa kuendelea kesho kwa mchezo mmoja utakaowakutanisha Coastal Union dhidi ya Kagera Sugar kwenye uwanja wa CCM Mkwakwani utakaopigwa majira ya saa 1 jioni.

Popular Posts

Exit mobile version