Akizungumza kwenye mkutano mkuu wa TFF Rais wa Shirikisho la soka nchini [TFF] Wallace Karia amesema fedha za zawadi za michuano ya vijana pamoja na ile ya mashule zina maelekezo ya matumizi yake na sio za kugawana.
Rais Karia ametoa ufafanuzi huo baada ya kuwepo kwa taarifa za wachezaji wa timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 15 kupewa posho ya elfu 20 na kunyang’anywa jezi baada ya kumalizika kwa mashindano nchini Uganda na kumaliza nafasi ya 3 iliyowafanya wapate zawadi ya dola elfu 75.
Karia amesema fedha hizo za zawadi kwenye mashindano ya vijana zimeelekezwa kuboresha miundombinu ya soka la vijana na sio fedha za kugawana kwa mujibu wa maelekezo ya Caf na Motsepe Foundation ambao wanatoa zawadi za mashindano ya mashule ambapo mwaka jana Fountain gate school walishinda zaidi ya dola laki nne.
Kwa kipindi cha miaka miwili soka la vijana nchini limeingiza zaidi ya dola laki 5 ambazo zimeelekezwa kujenga miradi ya maendelea kwa vijana.
Kuhusu kunyang’anywa jezi kwa vijana hao Rais Karia amesema kila kitu kina utaratibu wake na wangewezaje kugawa jezi hizo wakati mashindano mengine yanaendelea.
Hapo awali afisa habari wa TFF Cliford Ndimbo alinukuliwa akisema hundi ya fedha ya zawadi bado haijamature hivyo taratibu zikikamilika vijana hao watapata sehem ya mgao wa zawadi hiyo.