Yanga wamefanikiwa kupata ushindi wa kishindo wa mabao 3-0 dhidi ya Medeama kutoka Ghana kwenye mchezo ligi ya mabingwa Afrika, na kufanikiwa kuvuna alama 3 muhimu ikiwa ni ushindi wao kwanza wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa tangu mwaka 1998.
Wazo lilikuwa ni moja tu kwa Yanga, kupata ushindi kwenye mchezo huu. Na dhamira ya dhati kabisa ikionekana tangu dakika za mapema kabisa za mchezo, wakipeleka mashambulizi mfululizo langoni mwa Medeama.
Uhodari wa golikipa Kyei uliwaweka Medeama salama dakika ya 21 ya mchezo alipoupakua mpira uliokuwa ukielekea golini kwake baada ya kumgonga beki wake. Kona haikuweza kuzaa matunda.
Huku Maxi Nzengeli, Azizi Ki na Pacome Zouzoua wakionekana kupishana vizuri kama walivyozoeana, safu ya Ulinzi ya Medeama ikiongozwa na Babah Mussa na Emmanuel Cudjoe ilikuwa matatani.
Pengine silaha ya kujihami kwa Medeama ilikuwa ni kuupoza mpira hasa kwenye eneo la katikati, Manuel Mantey na Jean Vital Ourega walijitahidi kulifanya hilo lakini presha kubwa kutoka kwa Khalid Aucho na Mudathir Yahya kuliwanyima uhuru kutekeleza mpango kazi wao. Jambo lilirahisisha zaidi “MAP” kiushambuliaji kupatikana.
Dakika ya 33 ya mchezo, alikuwa ni Pacome Zouzoua aliyewainua Wananchi kwa bao la utaangulizi akitumia madhaifu ya walinzi wa Medeama, kuwapunguza na kisha kuachia shuti kali lililomshinda Felix Kyei. Yanga 1, Medeama 0.
Kila kitu kilianza kuonekana rahisi kwa upande wa Yanga licha ya Medeama kujaribu kurejea mchezoni wakijibu kwa mashambizi ya kushtukiza japo hayakuwa na macho sana.
Dakika ya 44, Kennedy Musonda alikosa goli la wazi akiwa kwenye kisanduku akipokea pasi elekezi kutoka kwa Mudathir Yahya lakini shuti lake likaenda nje ya lango.
Na hilo ndilo lilikuwa shambulizi la maana la mchezo huu kipindi cha kwanza, Yanga wakaenda mapumziko wakiwa mbele kwa kwa bao 1-0.
Kipindi cha pili Medeama walirejea na kasi ya kutaka kusawazisha goli wakicheza vizuri kwa kugongeana hasa eneo la kiungo na kupiga pasi za haraka za mashambulizi.
Dakika ya 54, Medeama walipata mkwaju wa Penati lakini Jonathan Sowah alikosa baada ya pigo lake kuokolewa na golikipa Djigui Diarra na pigo lake rejea likaokolewa pia.
Mchezo ulizidi kushika kasi huku timu zote zikishambuliana lakini wakiwa makini kwenye ulinzi. Lakini dakika ya 61, Bakari Mwamnyeto aliipatia Yanga bao la pili baada ya mpira alioupiga Kennedy Musonda kwa Kichwa akiunganisha mpira wa Kona kumgonga na kupoteza muelekeo Golikipa Kyei na mpira kujaa moja kwa moja wavuni. Yanga 2-0 Medeama.
Medeama wakaanza kuonekana kupoteza malengo huku goli la pili la Yanga likiwa limewavuruga na kujikuta wanapoteza sana mipira kwenye eneo lao na kufanya madhambi yasiyo lazima. Almanusura waadhibiwe tena na Bakari Mwamnyeto aliyeunganisha kwa kichwa mpira wa adhabu kubwa uliopigwa na Yao Kouassi lakini mpira ulipaa juu ya lango.
Mambo yalizidi kuwaendea kombo Medeama na Yanga kuwa kwenye siti ya mbele wakiumiliki mchezo watakavyo. Uzembe wa walinzi ulitumiwa vema na Azizi Ki aliyenyang’anya mpira na kisha kummpasia Mudathir Yahya aliyekwamisha kimiani bao la 3 kwa Yanga. 3-0 dakika ya 66.
Yanga wangeweza kupata magoli mengi zaidi pengine lakini ni kama walipunguza kasi labda kuridhika na walichokipata. Mabadiliko ya kumuingiza Sureboy na Kumtoa Pacome yaliakisi mpango wa Gamondi wa kuua matumaini yoyote ya Medeama ya kutengeneza mashambulizi yao. Hafiz Konkoni alitambulishwa pia mchezoni, Huku Skudu naye akichukua nafasi ya Azizi Ki.
Timu zote zilionekana kupungukiwa mipango kuelekea dakika hizi za mwisho wa mchezo kanakwamba wote waliridhika na matokeo yaliyopo. Mpaka dakika 90 zinatamatika, Yanga 3-0 Medeama.
Ushindi huu unawafanya Yanga kukwea mpaka nafasi ya 2 ya msimamo wa kundi D wakiwa na alama 5 sawa na vinara wa kundi hilo Al Ahly lakini wakiwa na mchezo mmoja pungufu.