Taifa Stars

STARS YAPOTEZA MISRI

Published on

Timu ya Taifa ya soka ya Tanzania, Taifa Stars imepoteza mchezo wake Kirafiki wa kujipima nguvu dhidi ya Misri kwa kufungwa mabao 2-0 kabla ya kuelekea Ivory Coast kwenye michuano ya AFCON.

Nidhamu ya kuwaheshimu Misri ilikuwa juu kuanzia dakika ya 1 ya mchezo, licha ya kuwa ni mchezo wa kirafiki lakini ni muhimu kwenye kujenga mpango kazi kuelekea AFCON. Misri ni timu kubwa.

Simon Msuva alionekana kusimama kama mshambuliaji pekee kwenye mfumo wa 4-2-3-1. Mbwana Samatta na Ben Starkie wakicheza Pembeni huku Feisal Salum akicheza namba 10 nyuma ya Msuva. Himid Mao na Mudathir Yahya kwenye moyo wa kiungo wa mfumo huu.

Mohamed Salah alipata nafasi ya kupiga shuti akipokea krosi kutoka Emam Ashour iliyowavuka walinzi wote wa Taifa Stars lakini shuti lake halikulenga lango.

Mbwana Samatta alijitengenezea nafasi ya kupiga shuti akipokea pasi ndefu kutoka Ibrahim Bacca lakini shuti lake lilipanguliwa vema na golikipa Mohamed Sobhi wa Misri.

Misri walipata bao la kwanza dakika ya 32 kupitia kwa Mohamed Trezegeut akipokea pasi elekezi kutoka kwa nahodha wake Mohamed Salah na yeye hakufanya ajizi akapishanisha mpira na Aishi Manula ambaye alikuwa ametoka langoni kujaribu kuzuia.

Mohamed Salah alipata nafasi ya kufunga bao la 2 kwa timu yake lakini shuti lake likambabatiza Bakari Mwamnyeto na mpira kuwa Kona.

Dakika ya 43, Marwan Attia alipiga shuti kali lakini Aishi Manula aliweza kupalaza shuti hilo kabla halijagonga mwamba wa juu kuliweka lango la Stars salama.

Taifa Stars walikuwa kwenye wakati mgumu dakika hizi za mwisho za kipindi cha Kwanza, wakipokea sana mashambulizi bila majibu.

Mapumziko, Taifa Stars walikuwa nyuma kwa bao 1-0.

Kocha Amrouche alifanya mabadiliko mwanzo wa kipindi cha pili akiwaingiza Tarryn Allarakhia, Charles M’mombwa, Haji Mnoga na Mohamed Omar Sagaf nafasi za Mudathir Yahya, Himid Mao, Simon Msuva na Ben Starkie.

Dakika ya 51, Nahodha Mbwana Samatta alipata majeraha na kushindwa kuendelea na mchezo nafasi yake ikachukuliwa na Kibu Denis.

Misri walipata bao la 2 kupitia kwa Mohamed Salah kwa njia ya mkwaju wa penati dakika ya 74 ya mchezo.

Kibu Denis alijitengenezea nafasi ya kuipatia Stars bao lakini shuti lake lilikuwa hafifu mikononi mwa Sobhi.

Taifa Stars walitengeneza tena nafasi nyingine kutokea pembeni, Mohamed Omar alipiga krosi ndani lakini Charles M’mombwa alishindwa kuiunganisha vizuri. Nafasi ya wazi kwa Stars walipoteza dakika ya 90+ ya mchezo.

Mohamed Salah alimtengenezea nafasi Mahmoud Kahraba lakini mpira wa kichwa ulipaa juu ya lango.

Dakika zote 90 za mchezo ulimalizika kwa Misri kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Taifa Stars.

Popular Posts

Exit mobile version