Timu ya Taifa ya Tanzania “Taifa Stars” inashuka dimbani hii leo kucheza mchezo wake wa kwanza wa hatua ya makundi dhidi ya timu ya Taifa ya Morocco majira ya saa mbili [20:00] usiku.
Taifa Stars ipo kundi F sambamba na timu za Taifa za Morocco, DR Congo na Zambia ambazo zote zinacheza leo, asilimia kubwa ya watu hawaipi nafasi Tanzania ya kufanya vizuri kwenye kundi hili.
Kuelekea mchezo huo kocha mkuu wa kikosi cha Taifa Stars Adel Amrouche amesema kuwa lengo lao kwenye mashindano haya ni kuiandaa timu kwaajili ya mashindano ya AFCON yajayo, yatakayofanyika Tanzania, Kenya na Uganda.
“Lengo letu ni kutengeneza timu ya baadae, tuna mipango ya baadae na shirikisho pia lina mipango ya baadae, na tunafanya kazi kwenye uelekeo huo”.
“Tanzania, Kenya na Uganda zinajiandaa kuwa wenyeji wa Afcon hicho ndicho kinailisukuma shirikisho kuandaa timu ya baadae”.
“Tupo hapa na tunafuraha kucheza na Taifa kubwa, na ni uzoefu mzuri kwa wachezaji wetu, tutaenda kupambana kadri ya uwezo wetu kuwaonyesha soka la baadae la Afrika Mashariki”, Kocha wa Stars Adel Amrouche alisema.
Nahodha wa timu ya Taifa ya Tanzania “Taifa Stars, Mbwana Ally Samatta amesema kuwa kambi ilikuwa nzuri na kila mchezaji ana morali ya kufanya vyema katika mchezo huo wa leo.
Samatta pia ameweka wazi kuwa wapo nchini Ivory Coast kwaajili ya kushinda AFCON kama ilivyo kwa timu zingine ambazo zinashiriki michuano hiyo.
Aidha Mbwana Samatta amesema asilimia kubwa ya kikosi kilichoitwa kwenye michuano hii ni vijana hivyo wanaiandaa timu itakayotumika kwenye michuano ya AFCON ambayo itafanyika nchiniTanzania sambamba na Kenya pamoja na Uganda.
“Tuna wachezaji wengi vijana, tupo hapa kuhakikisha tunasonga mbele kwenye michuano ya AFCON”.
“Tutashindana kadri tuwezavyo lakini pia tunaiandaa timu kwa ajili ya mashindano yatakayofanyika Afrika Mashariki kwa nchi za Tanzania, Kenya na Uganda mwaka 2027”, Nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta.
Matumaini ya kufuzu hatua inayofuata kwenye michuano hiyo kwa watanzania walio wengi hawana na pengine mchezo wa kesho dhidi Morocco unaweza kurudisha imani kwa wadau wa soka.