Morocco ndio lililokuwa Taifa la mwisho kutoka ukanda wa UNAF lililokuwa linatetea bendera ya Ukanda huo kabla na wenyewe kutupwa nje ya Mashindano na Afrika Kusini kwa mabao 2-0 kwenye mchezo wa mwisho kabisa wa raundi ya 16 bora AFCON 2023.
UNAF(UNION OF NORTH AFRICA FOOTBALL), ni Umoja wa Mataifa ya ukanda wa Afrika Kaskazini, Ukanda namba 1 kisoka Afrika wenye Maskani yake Tunis, Tunisia inayojumuisha mataifa matano(5), Morocco, Egypt, Algeria, Tunisia na Libya huku Rais wake wa sasa akiwa Abdelhakim El-Shelmani wa Libya ambaye chini yake ameshuhudia anguko la Mataifa ya Ukanda wake kuelekea Robo Fainali za AFCON 2023.
MOROCCO
Wakiwa wametoka kuweka Historia kwenye Kombe la Dunia kwa kuwa Taifa la kwanza kutoka Afrika(CAF) kufika hatua ya Nusu Fainali ya Kombe la Dunia tangu kuanzishwa kwake ilikuwa ikipewa nafasi kubwa sana kufanya vema pia kwenye michuano hii chini ya Kocha bora wa mwaka Afrika, Walid Regragoui.
Lakini isivyo matarajio wakajikuta wanaangukia pua kwa kuishia hatua ya raundi ya 16 bora baada ya kutolewa na Afrika Kusini. Wakiwa wameanza vizuri mashindano haya kwa kuwafunga Tanzania mabao 3-0, uwezo wao dhidi ya DR Congo kwenye sare ya 1-1 ilianza kutia shaka juu ya ubora wao licha ya kupata ushindi mchezo wa mwisho dhidi ya Zambia na kufuzu hatua ya raundi ya 16 bora. Pamoja na kuwa na Mastaa wengi kwenye timu, Morocco hawakuwa bora sana msimu huu wa AFCON.
EGYPT
Wakiwa hawajaambulia ushindi wowote ule msimi huu, wakiwa na Tofauti wa magoli 0 yani wakifunga Goli 7 na Kuruhusu 7 huku wakilala kwenye changamoto za mikwaju ya penati dhidi ya DR Congo kwenye hatua ya 16 bora, pengine huu ni miongoni mwa misimu ya ovyo kabisa ambayo Egypt wamewahi kupitia tangu mara ya mwisho watwae Ubingwa mwaka 2010.
Sare 3 za 2-2(dhidi ya Mozambique, Ghana na Cape Verde) kwenye hatua ya makundi pamoja na sare ya 1-1 dhidi ya DR Congo zilitosha kuwang’oa mabingwa hawa wa kihistoria wa AFCON huku wakiendelea kusubiri kutwaa ubingwa mwingine ikiwa imepita miaka 14 sasa tangu wafanye hivyo nchini Angola. Rui Victoria ana kibarua kigumu cha kuirejesha Egypt kwenye ubora wake huku sera yao ya “Protectionism” ikionekana kuelekea kufeli kutokana uzalishaji finyu wa vipaji vingine nchini Egypt.
ALGERIA
Shirikisho la Soka nchini Algeria halikona tabu kumfungashia Virago Kocha wao Djamael Belmadi, Kocha mzawa anayelipwa pesa nyingi kuliko wote barani Afrika, makadiri yakiwa takribani milioni 570 za Kitanzania kwa mwezi. Mkwanja mnene haswa lakini haukuendana na Matarajio ya waAlgeria akishindwa kuivusha timu yao hatua ya Raundi ya 16 Bora na kuishia makundi huku wakicheza vibaya sana kwenye kipigo cha 1-0 dhidi ya Mauritania na pengine wangeweza kufungwa zaidi kama Mauritania wangekuwa watulivu kutumia nafasi zao.
Wakimaliza wa Mwisho kwenye kundi, hii ni mara ya pili mtawalia Belmadi anaishia na Algeria yake hatua ya Makundi. Hajawa na muendelezo mzuri tangu atwae ubingwa huo wa AFCON msimu wa 2019. Wengi wakisema kuwa Kocha huyo amekuwa akicheza sana mechi nje ya uwanja kuliko ndani huku akihusika kwenye kauli kadhaa zenye utata. Kwa ukwasi wa wachezaji nyota kwenye kikosi, waAlgeria wanaamini Belmadi kawadhalilisha.
TUNISIA
Hawajawahi kuwa timu pendekezwa sana kwenye michuano yoyote hivi karibuni huku wengi wakiamini uwezo wao umeshuka, na hili wao wenyewe wamelithibitisha kwenye msimu huu wa AFCON wakimaliza nafasi ya mwisho kabisa kwenye msimamo wa kundi kama wenzao Algeria wakivuna alama 2 pekee.
Wakianza vibaya kampeni yao kwa kipigo cha 1-0 dhidi ya Namibia, Tunisia walienda kutoa sare ya 1-1 dhidi ya Mali lakini suluhu ya 0-0 dhidi ya Afrika Kusini ilimaanisha kuwa safari ya Tunisia imeishia pale. Tunisia wanatimiza miaka 20 tangu watwae ubingwa wa AFCON mwaka 2004 huku ikionekana kama vile hakuna ufufuo wowote wa hivi karibuni labda wabadili mifumo yao Huku Kocha Jalil Kadri aliyedumu kwa miaka miwili(2) tu akionekana kutokuwa muarobaini wa changamoto za timu ya taifa ya Tunisia huku Shirikisho la Soka likiwa halina Raisi tangu Wadie Jary akamatwe kwa kesi za rushwa na upangaji matokeo. Matokeo ya kiwanjani pengi ni tatizo moja tu ambalo Tunisia wanalo lakini kuna mengi zaidi wako nayo ikiwemo pia kuwa na mifumo finyu ya uzalishaji vipaji vingine kama yalivyo mataifa mengine ya ukanda huu.
LIBYA
HAWAKUSHIRIKI KABISA
Licha ya Raisi wa Shirikisho hili la soka la Libya kuwa pia ndiye Raisi wa Shirikisho la Ukanda wa UNAF Bw. Abdulhakim El-Shalmani, Libya bado ni taifa ambalo halina rekodi nzuri sana kwenye soka la Kimataifa. Sio tu kuwa timu pekee ya Ukanda huu ambayo haijawahi kushiriki Kombe La Dunia lakini tangu washiriki AFCON mwaka 2012 ikiwa ni mara yao ya 3 tu(zingine ni 1982 wakiwa wenyeji na 2006) hawajashiriki tena mpaka hii leo ikiwa ni miaka 12 imepita.
Licha ya kuwa na vilabu vinavyofanyaga vizuri kwenye michuano ya CAF kama Al Ahli Tripoli, vita za wenyewe kwa wenyewe zisizoisha zimekuwa ni moja ya kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya timu ya Taifa ya Libya. Itakumbukwa walicheza mechi yao ya AFCON 2012 dhidi ya Mozambique ilichezwa kwenye uwanja ukiwa hauna watu, Cairo. Kuna mengi ya kuwekwa sawa kabla ya Libya kurudi kuwa timu shindani.
Pengine tangu michuano hii iitwe AFCON mwaka 2002, hii ni mara ya 2 tu tunashuhudia michuano hii ikiingia hatua ya Robo Fainali bila ya kuwa na timu yoyote kutoka ukanda huu wa UNAF ambao umekua ukitamba sana miaka ya nyuma. Je hili ni anguko rasmi la utawala wao?