Nyota wa zamani wa timu ya Taifa ya England na klabu ya Manchester United kiungo Jesse Lingard amejiunga na klabu ya FC Seoul inayoshiriki Ligi kuu nchini Korea Kusini kwa mkataba wa miaka miwili, huu unakuwa usajili wa kwanza mkubwa kufanywa na klabu inayoshiriki Ligi ya Korea.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 31 amekuwa hana timu tangu alipoachana na klabu ya Nottingham Forest inayoshiriki Ligi kuu nchini England mwishoni mwa msimu uliopita.
“Nimekuwa nikihitaji changamoto mpya na kutengeneza kumbukumbu mpya kwenye kazi yangu, naamini kuwepo hapa Korea Kusini ni sehemu sahihi kwa hilo,” alisema Lingard.
FC Seoul inatumia uwanja wa Seoul World Cup na ni timu yenye mashabiki wengi kwenye Korean League na imeshinda taji la Ligi mara sita [6] na mara ya mwisho kutwaa taji hilo ni mwaka 2016.
Zaidi ya mashabiki 200 walijitokeza uwanja wa ndege wa Incheon kwaajili ya kumpokea Lingard wakati anawasili kukamilisha vipimo vya afya na mambo mengine mapema wiki hii.
“Nimepokea ofa nyingi sana tangu majira ya joto mwaka jana,” aliongeza Lingard.
“Klabu zingine zilileta ofa za mdomo, FC Seoul ilileta ofa ya maandishi, maafisa wa klabu walionyesha uhitaji wao kwa kuja Manchester kutazama hali yangu ya kimwili, kwa wakati huo nikaamua kusaini FC Seoul.”
Klabu hiyo ya FC Seoul inatarajiwa kuanza kutupa karata yake ya kwanza ya Ligi kuu nchini Korea mnamo March 2 dhidi ya klabu ya Gwangju, kwasasa Ligi hiyo bado haijaanza.