Azam FC wameshindwa kufurukuta mbele ya Nyuki wa Tabora baada ya kulazimishwa Suluhu ya 0-0 kwenye mchezo wa ligi kuu Tanzania Bara uliopigwa kwenye uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora huku Azam FC hawakuwa na hata shuti 1 lililolenga lango na Tabora United wakionyesha kandanda safi.
Tabora United walionekana kuanza kwa kasi kubwa kwenye mechi hii mara kadhaa wakimjaribu golikipa Mohamed Mustapha ambaye alikuwa imara langoni mwake mara zote.
Eneo la kiungo sana sana lilikuwa bize zaidi, Huku Kiungo Cletus Eba akifanya usambazaji mzuri wa mipira eneo la pembeni mwa kiwanja ambayo ndiyo ilikuwa njia ya kuanzishia mashambulizi akitumika zadi Yohana Mkomola na Banza Kalumba.
Azam wakionekana kutumia umbo la kuwa na washambuliaji watatu, Abdul Sopu, Kipre Junior na Gybrill Sillah bado hawakuonekana kuwa na makali mpaka dakika 30 za mwanzo huku pakiwa hakuna shuti lolote lililomtatiza John Nobel.
Kipindi cha kwanza hakikuweza kuzaa matunda yoyote, timu zote zikienda kupumzika bila goli lolote, 0-0.
Kipindi cha pili kilizidi kuwa bora kwa Tabora United wakiwalazimisha Azam kuwa timu ya pili kiwanjani.
Cletus Emoltan Eba alionekana kuwa mwiba mchungu kwa walinzi wa Azam, akitengeneza nafasi nyingi ambazo kwa bahati mbaya hazikuweza kutumiwa ipasavyo.
Azam walijaribu kuimarisha safu yao ya ushambuliaji kwa kuwaingiza Ayoub Lyanga, Prince na Iddy Selemani lakini bado hawakuweza kufua dafu.
Almanusura Jackson Mbombo aipatie timu yake ya Tabora United bao la ushindi dakika za mwisho kabisa za mchezo lakini golikipa Mohamed Mustapha alisimama imara.
Dakika zote 90 zikatamatika kwa suluhu ya 0-0 na baada ya mchezo, Kocha Mkuu wa Tabora United, Goran Kopunovic alisema
Najivunia sana timu yangu leo. Mimi natoka ulaya na nilitaka kuonyesha soka la Ulaya. Nilitaka kuwaonyesha Azam wachezaji wangu wana uwezo kiasi gani na leo walifanya kila kitu nlichowaelekeza kasoro tu hatukupata bao la ushindi. Naiona timu yangu ikiimarika na hivi karibuni tutaanza kuzikusanya alama 3.
Naye Kocha Msaidizi wa Azam FC, Youssouph Dabo alikuwa na haya ya Kusema
Sijafurahishwa na matokeo. Sijafurahishwa na kila kitu kuhusu timu yangu leo hasa eneo la ushambuliaji. Mechi nzima bila shuti la kulenga lango sidhani kama inavumilika. Lakini bado kuna michezo 14, kuna alama zingine nyingi za kupigania na tutaenda kujiandaa vizuri zaidi kwa ajili ya michezo ijayo.
Katika Hatua nyingine Kocha Dabo alitoa malalamiko yake kwa waamuzi
Kuna baadhi ya vitu tunavilalamikia kila siku lakini tunashangaa hatuoni mabadiliko. Ligi ya Tanzania ni miongoni mwa ligi Bora Barani Afrika, si ndio? Lakini kwanini kwenye AFCON hawajapeleka Waamuzi? Yani kuna nchi kama Somalia hata Rwanda zimepeleka waamuzi lakini sisi ambao ligi yetu ni Ligi bora zaidi hatujapeleka waamuzi, ni swali la msingi la kujiuliza. Kama kweli tunataka kusogea mbali zaidi, Waamuzi nao wasogee zaidi. Wawe bora pia.
Azam FC wanafikisha alama 36 wakisogea hadi nafasi ya 2 wakiwazidi Simba kwa tofauti magoli ya kufunga na kufungwa. Huku Tabora United wakisogea hadi nafasi ya 12 wakiwa na alama 17 sawa na JKT Tanzania walio nafasi ya 11 wakipishana kidogo kwenye magoli ya kufunga baada ya michezo 16.