Hillsborough ni eneo dogo lililopo South Yorkshire, nchini England, ni eneo ambalo klabu ya Sheffield Wednesday wanatokea huko.
Eneo hili lina uwanja uliojengwa mwaka 1899 na ulitumika kwaajili ya michezo mbalimbali ya Ligi pamoja na michezo ya FA.
Mwaka 1989 shirikisho la soka nchini England liliutangaza uwanja wa Hillsborough kuwa mwenyeji wa mchezo wa nusu fainali kati ya Nottingham Forest na Liverpool.
Shirikisho la soka nchini England liliuchagua uwanja huo kwasababu kati ya timu hizo mbili hakuna timu iliyokuwa inautumia hivyo ulikuwa ni “Neutral”.
Asubuhi ya April 15, 1989, ilikuwa siku ya mchezo mwenyewe, mashabiki walinunua sana tiketi kwaajili ya mchezo huo, Liverpool ilikuwa na mashabiki wengi zaidi, uwanja ulitarajiwa kuingiza mashabiki 53,000 pekee.
Sababu ya kuingiza idadi hiyo ni kuepuka uhuni, mashabiki wa timu zote mbili walielekezwa kupita kwenye njia tofauti za kuingia uwanjani.
Mashabiki wa Liverpool wenye tiketi za kuwa eneo la kusimama uwanjani walitakiwa kupita njia ya Leppings.
Mashabiki hao walitakiwa kupita kwenye Turntiles moja kati ya saba [Kwa wale waliofika uwanja wa Taifa au kivukoni kile kifaa unapoweka kadi kinafunguka unaingia ndio TURNTILES], kulikuwa na njia mbili za kuingia uwanjani ambazo zilikuwa zimefunguliwa.
Kutokana na uwepo wa turnstiles chache za kuingilia uwanjani, ilibidi kitengenezwe kizuizi kwa mashabiki 10,100 waliokuwa wanataka kuingia uwanjani kwenye jukwaa la watu wa kusimama [Watu wa Vibe].
Mchezo ulikuwa unachezwa saa tisa [03:00] Alasiri, lakini zikiwa zimesalia dakika 30 kabla ya mchezo kuanza zaidi ya nusu ya mashabiki walikuwa nje ya uwanja.
Akitumaini kupunguza msongamano, Mkuu wa polisi wa mji wa Yorkshire, David Duckenfield ambaye hakuwa na uzoefu wa usimamizi viwanjani Hillsborough, aliamuru geti C ambalo ni la kutokea lifunguliwe ili mashabiki waingilie ikiwa ni saa 2:52 Alasiri zikiwa zimesalia dakika nane mchezo kuanza.
Mashabiki 2,000 waliingia kupitia hilo geti na licha ya njia ya pembeni ilikuwa wazi lakini idadi kubwa ya mashabiki walikimbia kuelekea geti kuu, na tayari watu walikuwa wamejaa kwenye njia ya 3 na ya 4.
Wakati mashabiki wanakimbia kuelekea kwenye njia hiyo ajali kubwa ilitokea, inaaminika ilisababishwa na hasira za mashabiki kukaa nje ya uwanja kwa muda mrefu bila matumaini, hivyo watu wakakanyagana wakati wanaelekea lango kuu.
Maafisa wa sheria mwanzo waliamini kuwa tatizo lilisababishwa na mashabiki wakorofi na mchezo ukawa umesitishwa kabla ya dakika tano mchezo huo kuanza.
Mawasiliano mabovu na uratibu mbovu vilichangia kwaasilimia kubwa zoezi la uokozi kuwa na kasi ndogo, hivi ikabidi mashabiki wengine waungane na watoa huduma kuwasaidia wahanga wa tukio hilo.
Watu 97 waliuwawa na mmoja wa wahanga alifariki mwaka 1993 na mwingine aliyepata majeraha ya ubongo alifariki Dunia mwaka 2021, kwenye tukio hilo la kukanyagana watu zaidi ya 760 walijeruhiwa.
Baada ya janga hilo kutokea, polisi waliwalaumu mashabiki wa Liverpool kuhusiana na tukio hilo ambao walidaiwa kuwa walikuwa wamelewa na hawakutaka kufuata utaratibu.
Afisa mkuu wa polisi Duckenfield alidai kuwa mashabiki walilazimisha kufunguliwa kwa geti C. Ripoti ya mwaka 1989 ilieleza kuwa maafisa walifanya makosa, wakishindwa kufunga lango kuu baada ya jukwaa la 3 na la 4 kuwa limejaa.
Mwaka uliofuata uchunguzi ulifanyika na ikabainika kuwa hapakuwa na ushahidi wa kutosha kuleta mashtaka ya jinai.
Ripoti ya Coroner iliyotolewa mwaka 1991 inaeleza kuwa wote waliokufa walikuwa tayari wameshapita muda wa kuhudumiwa ilikuwa ishafika saa 3:15 Jioni ambapo Ambulance ya kwanza ilifika, kitu hicho kilizuia uchunguzi kufanyika hivyo vifo hivyo vikatafsiriwa kama ajali.
Uchunguzi ukaendelea tena na mwaka 2009 liliundwa jopo la kujitegemea kufanya uchunguzi wa tukio hili.
Miaka mitatu baadae jopo hilo lilitoa ripoti yao na kuonyesha kuwa polisi walihusika kwa kiasi kikubwa, na hapakuwa na ushahidi juu ya matumizi ya pombe au fujo kupelekea kutokea kwa tukio hilo na iliaminika pengine wangesaidia watu 41 kutoka kwa wale waliopoteza maisha kama kungekuwa na uokozi wa maana.
Uchunguzi huo ulianza tena mwaka 2014 na mwaka uliofuata Duckenfield alikiri kuwa alidanganya kuhusu mashabiki kufungua geti C.