Klabu ya soka ya AC Milan ya Italia imetoa kauli za kummsifia mshambuliaji wao Olivier Giroud kwa ushujaa wake kwenye mchezo dhidi ya Genoa pale alipochukua nafasi ya golikipa Mike Maignan ambaye alipewa kadi nyekundu huku Milan wakiwa wamemaliza idadi ya wachezaji kufanyiwa mabadiliko.
Giroud aliokoa hatari iliyokuwa ikilengwa golini kwao dakika za mwisho kabisa za mchezo na kuisadia timu yake kupata alama 3 muhimu. Milan wamesema kuwa kutokana na ushujaa wake wanafikiria kumuongeza kwenye orodha ya magolikipa wa timu lakini pia watatengeneza jezi maalumu ya golikipa yenye “Giroud 9” mgongoni na zitauzwa kwa mashabiki.
Kwa upande wa Giroud alisema
Sikuwahi kuwa na uzoefu kama ule. Ulikuwa ni wakati mzuri sana kwangu kuisaidia timu kupata matokeo. Nilipokuwa mdogo nilikuwa nikitumika kama golikipa wakati mwingine ndio maana nikachaguliwa. Niliumia kidogo pale lakini hakuna shida. Jezi hii nitaiweka kwenye fremu kama kumbukumbu.
Bachi ya kwanza ya jezi za “Giroud 9” tayari zimeshaingia mtaani na zimekwisha. Klabu iko kwenye mchakato wa kutengeneza zingine na kuziingiza sokoni.