Mapinduzi Cup

AZAM FC HIYOO ROBO FAINALI MAPINDUZI

Published on

Azam FC wamefanikiwa kufuzu hatua ya Robo Fainali ya mashindano ya Mapinduzi Cup baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya timu ya Vital’O kutoka nchini Burundi.

Azam walipata bao la utangulizi kupitia kwa mshambuliaji wake Alassane Diao akitumia makosa ya kimawasiliano kati ya mlinzi wa Vital’O Alfan Bigirimana na golikipa wake Ndayishimiye wakati wakitaka kuzuia pasi kutoka kwa Yannick Bangala na kuupachika mpira wavuni goli likiwa wazi.

Wakiwa kwenye umbo la 4-2-3-1, Huku pakiwa na mabadiliko ya baadhi ya wachezaji akiwemo Adolf Bitegeko anayekipiga nchini Iceland akicheza nyuma ya mshambuliaji kwenye safu ya viungo washambuliaji. Ayoub Lyanga na Iddy Nado wakicheza kwenye pembe.

Alassane Diao alikosa nafasi nyingine ya kuipatia Azam bao la pili akipokea pasi nzuri kutoka kwa Ayoub Lyanga. Licha ya kufanya utulivu kwenye kuandaa mpira, shuti lake lilikuwa hafifu.

Vital’O hawakuwa na makali sana dakika 45 za mwanzo japo walikuwa na baaadhi ya nyakati, wakipiga shuti 1 tu langoni.

Hali haikuwa tofauti kwa Azam pia kwani licha ya kumiliki sana mpira, nao walipoga mashuti mawili tu langoni ambalo 1 ndilo lililozaa goli pekee.

Dakika 45 za kwanza zilimalizika Azam wakiwa kifua mbele kwa bao 1-0 licha ya timu zote kuwa kwenye uwiano usiopishana sana kwenye kumiliki mpira na kiuchezaji lakini hapakuwa na shinikizo kubw hasa eneo la mwisho.

Vital’O walirejea vema kipindi cha pili ukitumiwa zaidi upande wa kulia wa Vital’O anakocheza Hussein Kwizera lakini upande wa kushoto wa Azam anakocheza Paschal Msindo.

Azam FC walijibu mapigo dakika ya 57, baada ya Alassane Diao kupachika bao la 2 kwa timu yake ya Azam akimalizia kazi nzuri ya Ayoub Lyanga kwa mtindo wa kichwa mchupio. Hili lilikuwa ni bao la 3 kwa Alassane Diao kwenye michuano hii.

Vital’O walirudisha bao 1 kwa mkwaju wa penati dakika ya 63 kupitia kwa Jean Nzeyimana baada ya mchezaji wa Vital’O kuchezewa madhambi na Ayoub Lyanga kwenye eneo la hatari. 2-1.

Azam waliamua kuingiza nguvu mpya kwa kuwapumzisha Iddy Nado, James Akaminko na George William na nafasi zao kuchukuliwa na Malickou Ndoye eneo la ulinzi, Kipre Junior na Prince Dube nao wakiingia eneo la Ushambuliaji na kubadili mfumo kuwa 4-4-2. Ayoub na Kipre wakicheza kama mawinga na Dube na Alassane Diao kama washambuliaji.

Mabadiliko hayakuchelewa kuzaa matunda kwani dakika ya 72 tu, Azam walipata bao la 3 kupitia kwa Pascal Msindo akimalizia kazi mujarab ya Kipre Jr akiwapunguza walinzi wa Vital’O kabla ya kutoa pasi kwa mfungaji.

Azam waliendelea kuumiliki mchezo kwa dakika zilizobakia wakicheza kwa kasi sana eneo la ushambuliaji huku Bitegeko akilimiliki sana eneo la kiungo. Kiwango kingine cha kuvutia kikionyeshwa na Paschal Msindo.

Mpaka mpira unamalizika, Azam 3-1 Vital’O. Azam wakiongoza Kundi na kukata tiketi ya robo fainali.

Mchezaji bora wa Mechi akitangazwa kuwa Alassane Diao wa Azam FC akichukua tuzo hii kwa mara ya pili mfululizo huku Mchezaji mwenye nidhamu akichaguliwa kuwa Hussein Ndayishimiye wa Vital’O ya Burundi.

Popular Posts

Exit mobile version