Mapinduzi Cup

SIMBA YATAKATA UWANJA WA AMAAN

Published on

Simba SC wamefanikiwa kuvuna alama 3 muhimu baada ya kuifunga timu ya Singida FG kwa mabao 2-0 na kukwea kileleni mwa msimamo wa Kundi B.

Kasi ya Simba aliyoanza nayo ilisababisha kona ya mapema tu dakika ya 2 baada ya Willy Essomba Onana kupiga shuti lililombabatiza bekibwa Singida FG, Biemes Carno. Lakini kona haikuzaa matunda.

Simba walikuwa kwenye umbo la 4-3-3 leo tofauti na 4-2-3-1 iliyozoeleka huku watatu kwenye kiungo wakiwepo Fabrice Ngoma, Sadio Kanoute na Hamisi Abdallah. Huku safu ya ushambuliaji wakicheza Moses Phiri, John Bocco na Willy Essomba Onana.

Singida FG walikuwa kwenye mfumo wao ule ule wa 4-2-3-1. Habibu Kyombo na Deus Kaseke pembeni huku Duke Abuya akicheza nyuma ya Elvis Rupia. Wahimili wawili wa mfumo wakiwa Morice Chukwu na Yusuf Kagoma.

Dakika ya 27 John Bocco alipoteza nafasi ya wazi kabisa baada ya Kiungo Morice Chukwu kutoa pasi fyongo kwa golikipa wake Ibrahim Rashid Parapanda lakini alifanya kazi ya ziada kuepusha madhara golini kwake.

Mpira wa krosi ya Duke Abuya ulionekana kama hauna madhara lakini ulitua kichwani mwa Habibu Kyombo lakini Ally Salim aliokoa hatari hiyo.

Mechi iliendelea kushika kasi huku kila timu ikishambulia kwa wakati wake. Licha ya kwamba ilianza taratibu kwa Singida lakini walianza kuonyesha hatari yao hasa wanapofika langoni mwa Simba.

Moses Phiri alipata nafasi ndani ya sanduku la Singida FG akipokea pasi maridadi kutoka kwa Fabrice Ngoma lakini Ibrahim Parapanda alikuwa sambamba na shuti lake.

Singida FG walidhani wamepata goli dakika ya chache kabla ya kwenda mapumziko. Shuti kali la Elvis Rupia akitumia pasi nzuri kutoka kwa Deus Kaseke aliyepokea pasi fyongo kutoka kwa Israel Mwenda liligonga mwamba wa juu lakini mpira haukuvuka mstari wakati unatua chini kama ilivyong’amuliwa na muamuzi msaidizi, Ibada.

Mapumziko timu zote zikaenda zikiwa hazijafungana.

Simba waliingia kipindi cha pili na mabadiliko kadhaa akitoka John Bocco na Kuingia Jean Baleke huku Luis Miquissone na Mohammed Mussa wakichukua nafasi za Moses Phiri na Abdallah Hamisi. Huku pia mfumo ukibadilika na kurudi kuwa mfumo mama wa 4-2-3-1.

Na dakika ya 47 tu, Essomba Onana alifanyiwa madhambi nje kidogo ya eneo la hatari la Singida. Yeye mwenyewe akapiga mpira huo wa adhabu uliokwenda moja kwa moja nyavuni ukimshinda Parapanda. Simba 1-0 Singida FG.

Willy Essomba Onana alipata nafasi nyingi ya pigo huru lakini safari hii Parapanda alimkatalia.

Ally Salim alifanya moja ya uokovu bora wa mechi baada ya kuzuia mpira wa kichwa uliounganishwa na Elvis Rupia kutokana na mpira wa Kona, wakati mpira ukionekana unaelekea nyavuni, Ally akaupangua na kuwa Kona.

Dakika ya 59 ya mchezo, Luis Miquissone aliwakumbusha wana Simba kuwa yupo baada ya kuunganisha kwa shuti kali pasi ya Shomari Kapombe kutokea pembeni, nje ya eneo la penati la Singida FG na mpira kutinga wavuni kuwapatia Simba bao la 2. 2-0 kwa Simba.

Fancy Kazadi, Meddie Kagere na Dickson Ambundo walitambulishwa kwenye mchezo na Singida FG ili kuongeza kasi ya mashambulizi kidogo wakienda nje Duke Abuya, Elvis Rupia na Habibu Kyombo. Lakini pia Amos Kadikilo akimpokea Yahya Mbegu.

Simba waliendelea kuutawala mchezo kwa kiasi kikubwa licha ya Singida kuwa na baadhi ya nyakati.

Dakika zote 90 zikamalizika kwa Simba kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Popular Posts

Exit mobile version