Mapinduzi Cup

MLANDEGE WATANGULIA NUSU FAINALI MAPINDUZI CUP

Published on

Timu ya soka ya Mlandege imefanikiwa kufuzu hatua ya Nusu Fainali ya mashindano ya Mapinduzi Cup baada ya kuwatoa ndugu zao KVZ kwa changamoto ya mikwaju ya penati kwenye mchezo uliomalizika 0-0 baada ya dakika zote 90.

Mechi ilikuwa na ufundi mwingi sana huku Mlandege wakionekana kuutawala mchezo hasa kwenye eneo lao la kiungo licha ya kwamba timu zote zilikuwa zikicheza kwa tahadhari kubwa.

Kutokuanza kwa Mustafa Muhsin leo kwenye eneo la kiungo la Mlandege kulimaanisha kuanza kwa Diego Fernando na mfumo kuwa 4-3-3. Diego akiwa sambamba na Abdallah Kulandana na Emmanuel Pious. Kimani Armouni, Khor Bennet na Abdallah Pina waliongoza mashambulizi.

KVZ walianza na 4-4-2 akionekana Sabri Dahal kutokea upande wa kulia huku Mathias akitokea upande wa kushoto kuwapatia huduma washambuliaji viongozi, Akram Mhina na Halifa. Walionekana kuzidiwa kwenye eneo la kiungo kutokana na kuwa na viungo wawili tu Yusuf Mfaume na Mohammed dhidi ya viungo watatu wa Mlandege.

Abdallah Pina alipata nafasi ya kuunganisha krosi nzuri ya Khor Bennet lakini kichwa chake hakikulenga lango na kupaa juu.

KVZ Walikuwa karibu kupata goli kupitia kwa Yusuf Mfaume lakini shuti lake lilidakwa na golikipa Athuman

Mohammed alipata nafasi nyingine ya kuachia shuti kali lakini lilipaa juu ya lango.

Pamoja na yote hayo hapakuwa na matukio mengi ya hatari ya kuripoti mpaka mapumziko timu zote zikienda vyumbani pakiwa hakuna aliyepata bao.

Suleiman Mwalimu na Gaby Fundumo waliingia upande wa KVZ kipindi cha pili.

Gaby Fundumo aliachia shuti kali langoni mwa Mlandege lakini golikipa Athuman Hassan aliokoa shuti hilo na kuliweka lango lake salama.

Mlandege nao walifanya mabadiliko akiingia Optatous Lupekenya na Yusuf Suleiman Jusa wakichukua nafasi za Kimani Arbouni na Diego Fernando.

Dakika ya 63 Akram Mhina wa KVZ alipata nafasi nzuri ya kufunga baada ya mabeki wa kati wa Mlandege Maliek Zidan na Mohdy kujichanganya lakini shuti lake lilikuwa hafifu.

Optatous Lupekenya alikitengenezea nafasi nzuri akiwa katikati ya walinzi wa KVZ kwenye eneo la penati lakini alikosa umakini wa umaliziaji. Dakika ya 75, bado 0-0.

Gaby Fundumo alimuona Suleiman Mwalimu na kumpigia pasi safi kabisa naye aliutuliza kwa utulivu wa aina yake lakini alishuhudia shuti lake likienda kugonga nguzo. Nafasi nyingine ilipotea kwa KVZ.

Mlandege nao walifanya shambulizi la hatari kupitia kwa Optatous Lupekenya aliyegongeana vizuri na Kohr Bennett lakini shuti lake libabatiza walinzi wa KVZ.

Dakika zote 90 zilitamatika kwa suluhu ya 0-0 na mechi kuingia kwenye changamoto ya mikwaju ya Penati ili kumpata mshindi.

Mlandege waliibuka na ushindi kwa Penati 3-2.

Waliopata upande wa KVZ walikuwa ni Khalifa Hassan na Bashiri Iker huku Waliokosa ni Salim Hamisi Salum, Dudu na Mohammed.

Waliopata upande wa Mlandege walikuwa Kohr Bennett, Emmanuel Pious, Yusuf Suleiman Jusa huku Waliokosa ni Abdallah Nassor, Abdallah Pina.

Mchezaji bora wa Mechi Hii alikuwa ni Mlinzi Salum Athumani wa KVZ.

Mchezaji mwenye nidhamu alichaguliwa kuwa Masoud Rashid wa Mlandege.

Popular Posts

Exit mobile version