Kocha Msaidizi wa Singida Fountain Gate, Nizar Khalfan amesema mechi ya kesho dhidi ya Simba haitakuwa rahisi, lakini ana uhakika wa ushindi kwa maandalizi waliyofanya.
Mbele ya wanahabari leo, Nizar ameweka wazi kuwa hawaitazami kama mechi ya kisasi bali wanachojua ni kwenda kushinda.
“Hata wao wanajua shughuli yetu, wakikutana na sisi huwa si mechi ya kitoto na wangeambiwa wachague kati yetu na Azam kwenye hatua hii nadhani wangechagua kukutana na Azam na siyo Singida”.
Nizar ameweka wazi kuwa kama timu hizo zikifika kwenye mikwaju ya Penalty basi wanauhakika Simba itatoka kwa mikwaju ya penalty.
“Kama tukitoka sare dakika 90 , basi wao watatoka kwa penati”.
Kuhusu ‘utajiri’ wa washambuliaji walionao, Nizar amesema haiwapi ugumu benchi la ufundi bali inawarahisishia kazi kwakuwa yeyote anayeanza anatimiza wajibu wake, jambo ambalo ni hamasa kwa wanaoanzia benchi.
Aidha kocha huyo amesema hawawezi kutoa siri ya kile kinachowapa kiburi cha kuifunga Simba hapo kesho.
“Hatuwezi kutoa siri”.
Singida Fountain Gate na Simba hii itakuwa ni mara ya pili kukutana kwenye michuano hii, ikiwa mara ya kwanza walikutana kwenye hatua ya makundi na Simba ikashinda goli 2-0.