Sapraizi waliokuja nayo Equatorial Guinea iliwalizimu Wenyeji Ivory Coast kusubiri mpaka mechi za mwisho kujua hatima yao ya kufuzu raundi ya 16 bora. Wakishinda mchezo mmoja(1) tu kati ya mitatu na kuambulia kipigo cha kudhalilishwa cha 4-0 kutoka kwa Equatorial Guinea kwenye mchezo wa mwisho, kiliwaweka hatiani.
Nigeria nao walihitaji matokeo ya Ushindi dhidi ya Guinea Bissau na Asante kwa goli kwa la kujifunga la Opa Sangante, liliwapa tiketi Nigeria kwa kupata ushindi mwembamba wa 1-0 kwenye mechi yao mwisho.
KUNDI B
CAPE VERDE, EGYPT
Cape Verde walionekana ni kama wasindikiza kundi kwenye kundi hili huku wengi wakiamini njia ni nyeupe sana kwa wababe, Ghana na Egypt kwenye kundi hili lakini wamba hawa walikuja kuharibu utaratibu wa kawaida huku wakiwatoa kamasi wababe wote wawili, wakiwanyuka Ghana na kuwabana mbavu Egypt kwenye mchezo wa mwisho kwa sare ya 2-2 na kuongoza kundi hilo kibabe wakifikisha alama 7.
Ghana, licha ya kuwa timu iliyotabiriwa makubwa chini ya Kocha Chris Hughton huku pakiwa na nyota wengi kama Mohamed Kudus, Inaki Williams n.k, walijikuta wanaangukia pua kwenye kundi hili wakimaliza na alama 2 pekee huku wakikosa hata nafasi ya “Best looser”.
KUNDI C
SENEGAL, CAMEROON, GUINEA
Baada ya Kunyukwa kisawasawa kwa mabao 3-1 na Senegal, Cameroon ilihitaji vitu vitatu ili kufuzu kucheza hatua ya raundi ya 16 moja kwa moja, Mosi ni Biti kali kutoka kwa Rais wa FECAFOOT, Samuel Eto’o Fils, Pili Senegal Kumfunga Guinea na Tatu wao wenyewe wapate Ushindi kwenye mechi yao ya Mwisho dhidi ya Gambia. Na yote yalienda sawa yakisindikizwa na Maombi waliyoyafanya Kanisani siku 1 kabla ya mchezo wao wa mwisho.
Licha ya goli la 2 lililofungwa na Ilman Ndiaye nyota anayekipiga kwenye klabu ya Olympique Marseille ya kule Ufaransa kuonekana kama kutaka kuzima ndoto za Guinea lakini mwishoe na wao walifanikiwa kupenya kama washindi wa 3 bora.
KUNDI D
ANGOLA, BURKINA FASO, MAURITANIA
Nahodha Yali Dellahi wa Mauritania hakuwepo Kabisa kwenye Mechi waliopoteza kwa mabao 3-2 dhidi ya Angola, lakini alirejea kikosini na kufunga bao muhimu dhidi Algeria, bao ambalo sio tu lilivunja mioyo ya Waalgeria chini ya Kocha ghali barani Afrika, Djamel Belmadi lakini pia liliandika Historia kubwa kwa Taifa la Mauritania. Kutawala kwa Vilio uwanjani vilitosha kuelezea. Ushindi wa 1-0 wa Mauritania ulimaanisha kuwa Safari ya Algeria ilikomea hapo wakibaki na alama zao 2, Mauritania wakiungana na Angola na Burkina Faso ambao mechi yao kumalizika kwa ushindi wa 2-0 kwa Angola kulimaanisha wote wawili wanasonga hatua inayofuata.
KUNDI E
MALI, AFRIKA KUSINI, NAMIBIA
Baada ya kuchabangwa mabao 4-0 na ndugu zao, majirani wa ukanda mmoja wa COSAFA,Afrika Kusini, Ndugu hawa bado walihakikisha wanabebana kuingia raundi ya 16. Namibia kujitutumua mbele ya Mali kwenye mchezo wa mwisho huku Afrika Kusini akihakikisha anatamatisha Safari ya Tunisia kwa kumbana mbavu kwa suluhu ya 0-0, kulimaanisha kuwa Namibia anaungana na Afrika Kusini na Mali. Heshima ya COSAFA ikalindwa vema.
KUNDI F
MOROCCO, DR CONGO
Zilihitajika mechi za mwisho za kundi hili kuamua nani na nani wanasonga na akina nani wanabaki. Zambia akihitaji kupata Ushindi dhidi ya Morocco ili kujihakikishia kufuzu raundi ya 16 bora huku DR Congo akipapatuana na Tanzania wote wakijua kuwa anayeshinda mchezo huo ana nafasi ya kusonga.
Licha ya kucheza vizuri, Tanzania walishindwa kufua dafu mbele ya wakongomani ambao tayari walishafahamu matokeo ya Zambia kunyukwa na Morocco hivyo Karata ilikuwa mikononi mwao. Kumaliza na alama 2 kwa Zambia na Tanzania kulimaanisha kundi hili halitoweza kuwa na “Best Looser”. Sio Egypt pekee waliofuzu kwa kupata Sare 3, hata DRC wamo.
UFAFANUZI
Timu zilizofuzu kwa njia ya RANKING OF 3RD PLACED TEAMS zilifuzu kwa kuangaliwa Alama walizokusanya timu zilizomaliza nafasi ya 3 kwenye makundi yote 6.
Ghana na Zambia walishindwa kufika Timu 4 kati ya 6 kutokana na alama chache(2) walizomaliza nazo.
Timu hizo 4 zinaungana na timu 12 zilizofuzu moja kwa moja kwa kushika nafais ya 1 na ya 2 kwenye makundi yao ili kupata timu 16 za kucheza hatua ya mtoano kuanzia Raundi ya 16 Bora inayotarajiwa kutimua vumbi kuanzia Jumamosi ya tarehe 27/01/2024.