Mechi ilikuwa na rapsha nyingi sana hasa dakika za mwanzo, kila timu ikionyesha uchu wa kutafuta bao la mapema.
Azam wakicheza kwenye umbo la 3-4-3. George William, Edward Manyama na Yannick Bangala wakicheza kama mabeki wa tatu wa nyuma Nathaniel Chilambo upande wa kulia na Pascal Msindo upande wa kushoto kwenye safu ya wanne ikikamilishwa na James Akaminko na Mahmoud Haji. Safu ya ushambuliaji ikiwa na Ayoub Lyanga, Prince Dube na Alassane Diao.
Kwa dakika nyingi za kipande cha kwanza ni Mlandege ndio walioonekana hai zaidi kwenye mashambulizi. Dakika ya 23, Abdallah Iddy alishindwa kumalizia vizuri krosi iliyopigwa kutokea upande wa kulia wa Abdallah Said Ally na kuupaisha mpira huo.
Mlandege walikosa tena nafasi nyingine ya wazi baada ya beki Kijana George William kuteleza na mpira kumdondokea Optatus Lupekenya aliyepiga shuti lakini likaenda nje kidogo ya lango.
Bundi bado aliendelea kulisakama goli la Azam, dakika ya 32 ya mchezo Jamali alipiga krosi murua eneo la Azam lakini kichwa alichopiga Abdallah Iddy kikapaa juu ya lango.
Azam walizidi kuishi kwa hatari ndani ya dakika hizi 35 za mwanzo. Lakini Abdallah Iddy ni kama hakuwa na siku nzuri kazini. Dakika ya 35 alipenyezewa pasi elekezi na Optatus Lupekenya lakini umaliziaji ukwa finyu na mpira kupaa juu ya lango.
Almanusura Azam wajipatie bao la kuongoza kupitia kwa Yannick Bangala aliyeunganisha kwa kichwa kona iliyochongwa na Ayoub Lyanga lakini Abdallah Said Ally aliokoa akiwa kwenye mstari wa goli. Pengine shambulizi bora pekee la Azam mpaka dakika ya 43.
Mapumziko timu zote zilienda suluhu ya 0-0 huku Mlandege wakionekana kuwa na dakika 45 bora kuliko Azam.
Mchezo uliendelea kuwa wazi kwa timu zote. Azam wakisukuma mashambulizi huku Mlandege nao wakijibu. Mlandege walionekana tu kukosa utulivu hasa safu ya ushambuliaji.
Timu zilifanya mabadiliko kwenye maeneo yao muhimu, Azam wakibadili upande wa kushoto kwa kumuingiza kijana mwingine Abdallah Omary. Mlandege walijaribu pia kuboresha safu yao ya ushambuliaji lakini bado hapakuwa na nafasi nyingi za wazi kipindi hiki.
Dakika zikayoyoma na hatimae kila timu ikaonekana kama kuridhika na matokeo yaliyopo. Azam wakionekana kuwa chini kwenye mipango yao huku wakiwaruhusu Mlandege kujiamini zaidi na kucheza soka safi.
Dakika zote 90 zikamalizka bila kuwa na mbabe. Mchezo huu wa kundi A ukitamatika kwa Suluhu ya 0-0.
Kama kuna namna yoyote Azam wana dhamira ya kutwaa ubingwa wa michuano hii msimu huu basi wana mengi ya kurekebisha lakini utawasifu Mlandege kwa mchezo mzuri na ushindani waliouonesha.