Mapinduzi Cup

SINGIDA FG YAANZA KWA USHINDI, MR. MAPINDUZI AKITUPIA.

Published on

Singida FG wameanza vizuri michuano ya Mapinduzi baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya JKU huku mshambuliaji aliyetamba kwenye michuano iliyopita, Fancy Kazadi akifunga bao moja.

Singida FG walianza kutangaza uwepo wao kwenye mashindano na dakika za mwanzo tu wakalisakama sana goli la JKU, dakika ya 18 tu Elvis Rupia alikosa nafasi ya wazi kuitanguliza timu yake ya Singida FG baada ya shuti lake kummbabatiza golikipa wa JKU.

Haikuchukua muda sana Elvis Rupia kufuta makosa yake kwani dakia ya 21 tu alimalizia kazi nzuri ya Habibu Kyombo akitokea wingi ya kulia na kupiga krosi ndani iliyomkuta mfungaji. 1-0 Singida FG.

Singida FG walikuwa mzigo mzito sana kwa JKU ambao walionekana kutocheza vizuri sana huku wakishindwa kabisa kutengeneza nafasi zozote za wazi mbele ya walinzi wa Singida wakiongozwa na Joash Onyango na AbdulMajid Mangalo.

Habibu Kyombo alikuwa kwenye kiwango bora sana, dakika ya 36 alijitengenezea nafasi na kupiga shuti kali lakini golikipa alikuwa sawia nalo.

Mfumo wa 4-2-3-1 walioutumia Singida FG leo ulimuweka Habibu Kyomba na Deus Kaseke kwenye wingi za pembeni huku Marouf Tchakei akicheza nyuma ya mshambuliaji pekee, Elvis Rupia. Safu hii ya ushambulizi ilikuwa inalindwa na Duke Abuya na Morice Chukwu. Timu ilionekana iko kwenye mzani mzuri huku pia wakitumia ukubwa wao.

Wangeweza kuwa mbele kwa mabao mengi kama safu ya ushambuliaji yao ingekuwa inashirikiana vema kwa kupasiana lakini kuna muda ubinafsi uliwazidia.

Mapumziko Singida FG walienda Kifua mbele wakiwa na uongozi wa bao 1-0 huku pakiwa hakuna takwimu ya maana upande wa JKU.

Kama ilivyokuwa kipindi cha kwanza, Singida FG waliendeleza walipoishia na mapema tu dakika ya wakaandika bao la pili kupitia kwa Elvis Rupia. Goli la pili kwake na la 2 kwa timu yake usiku huu.

JKU Walifanya mabadiliko kipindi hiki cha pili wakiingiza wachezaji wenye uwezo na kasi zaidi kwenye safu ya ushambuliaji. Mchezo kidogo ulianza kuwa hai upande wa JKU.

Dakika ya 60, JKU walipata mkwaju wa penati baada ya Nahodha Gamba Iddy kufanyiwa madhambi na Kelvin Kijiri. Salehe Hamisi Abdallah alifunga penati kiufundi kabisa na kuirudisha timu yake mchezoni. JKU 1-2 Singida FG.

Singida FG nao walifanya mabadiliko kwenye safu yao ya ushambuliaji wakiwatoa Elvis Rupia, Habibu Kyombo na Deus Kaseke wakiingia Fancy Kazadi, Meddie Kagere na Dickson Ambundo. Lakini pia wakiimarisha safu ya Ulinzi kwa kumuondoa Kiungo mmoja Duke Abuya na kumuingiza beki Hamadi Waziri. Muda huo JKU nao walifanya mabadiliko.

JKU waliendelea kucharuka na kupeleka mashambulizi mfululizo kwa Wapinzani wao. Ikiakisi zaidi kwanini Mwalimu Thabo aliamua kuimarisha safu yake ya ulinzi. Utulivu tu ulikuwa ukikosekana kwenye eneo la mwisho. Parapanda akionyeshwa kadi ya njano kwa kuchelewesha muda.

Utatu wa Singida FG ulioingia kipindi cha pili uliamsha mashambulizi. Na walidhani wamepata goli la 3 dakika ya 79 kupitia kwa Fancy Kazadi ambaye alimalizia kwa kichwa mpira wa pigo huru uliochongwa na Marouf Tchakei na kupanguliwa na golikipa Yakub. Lakini muamuzi alisema kuwa golikipa kafanyiwa madhambi.

Lakini Singida walirudi tena dakika ya 81. Fancy Kazadi alipora mpira na kummpasi Dickson Ambundo ambaye naye alipiga pasi murua kwa Marouf Tchakei aliyeusogeza tu kwa Meddie Kagere aliyeukwamisha mpira kimiani na kuiandikia timu yake bao la 3.

Hawakuishia hapo, wakati JKU Wakijiuliza wamepigwaje hapo, Singida walisema bado hawajasema. Pasi safi kutoka kwa Meddie Kagere ikammkuta Kelvin Kijiri ambaye akapiga pasi elekezi ndani ya eneo la goli na kumkuta Fancy Kazadi, Mr. Mapinduzi aliyeiandikia Singida FG bao la 4. Dakika ya 86, JKU 1-4 Singida FG.

Singida FG wakautawala mchezo tena na kufanya walichotoka huku wakihakikisha hawawapi mianya ya aina yoyote JKU dakika za mwisho za mchezo.

Dakika 90 zinatamatika na Singida FG wanapata ushindi mnono wa mabao 4-1. Ushindi mkubwa hadi hivi sasa tangu michuano hii ianze.

Popular Posts

Exit mobile version