Mapinduzi Cup

KVZ YAIBANA MBAVU YANGA

Published on

Yanga wameshindwa kufurukuta mbele ya Vijana wa KVZ baada ya kulazimishwa Suluhu ya 0-0 kwenye mchezo wa Kundi C wa mashindano ya Mapinduzi Cup.

Jonas Mkude, Denis Nkane na Crispin Ngushi walikuwa katikati ya Vijana wengi wa Kikosi cha Vijana cha Yanga kwenye mechi hii dhidi ya KVZ.

Mchezo haukuonekana kuwa wenye kasi sana dakika 15 za mwanzo huku kila timu ikiamua kuuchezea tu mpira kuliko kufanya mashambulizi mengi ya hatari. Wote walikuwa na amani kukaa na mpira.

Dakika ya 17, Isack Emmanuel alipiga krosi nzuri kutoka upande wa kulia lakini kichwa cha Denis Nkane kiligonga nguzo ya juu na kwenda nje. Nafasi ikapotea kwa Yanga.

KVZ walidhani wamepata bao la utangulizi dakika ya 31 ya mchezo lakini kibendera cha Muamuzi msaidizi namba 2 tayari kilikuwa juu wakati mfungaji anafunga.

Hapakuwa na matukio mengi ya kuripoti katika dakika 45 za kwanza lakini ni KVZ ndio waliotengeneza nafasi angalau za kuwa karibu na kupata bao lakini walikosa umakini.

Mapumziko, KVZ 0-0 Yanga.

Yanga walifanya mabadiliko kipindi cha pili akitambulishwa mchezoni Usajili mpya Augustine Okra sambamba na Jesus Moloko, Kibwana Shomari na Joyce Lomalisa ili kuongeza nguvu na kasi ya mchezo.

Hata hivyo KVZ bado walionyesha utulivu wa hali ya juu, wakipambana kuzuia mashambulizi ya Yanga lakini na wao wakitengeneza nafasi wakiwa na mpira.

Augustine Okrah alipata majeraha dakika ya 64 ya mchezo na nafasi yake kuchukuliwa na Farid Mussa baada ya kushindwa kuendelea na mchezo.

Dakika ya 77, KVZ walikosa nafasi nzuri ya kupata goli kupitia kwa Akram lakini utasifu pia kazi nzuri ya mlinda lango Awesu Kassim aliyepangua vizuri shuti lake kabla ya mabeki wake kuokoa.

Yanga katika upande wa pili nao walikosa goli baada ya Crispin Ngushi kushindwa kumalizia vizuri krosi ya Farid Mussa dakika ya 78.

Mechi ilianza kushika kasi haswa kipindi hiki cha pili, licha ya Yanga kujaribu kuonyesha ukubwa wao lakini ni KVZ ndio walitengeneza nafasi nyingi za wazi kabisa. Pengine wangeweza kuwa mbele kwa zaidi ya goli 2 hata kama wangekuwa makini na nafasi zao.

Mechi iliendelea kuwa kwenye mzani sawa mpaka dakika za mwisho za mchezo huku hata kiu ya kutafuta magoli ikapungua.

Dakika zote 90 zikatamatika kwa matokeo ya 0-0.

Kwa matokeo hayo Yanga wanafanikiwa kufuzu hatua ya robo fainali baada ya kufikisha alama 7 kwenye mechi 3 walizocheza, wataungana pia na KVZ ambao nao wamefuzu wakifikisha alama 5.

Mchezaji bora wa Mechi alichaguliwa kuwa wa KVZ huku Mchezaji mwenye nidhamu akichaguliwa kuwa Jonas Mkude wa Yanga.

Popular Posts

Exit mobile version