Nyota mpya wa klabu ya Yanga Augustine Okrah jana kwenye mchezo wa kombe la Mapinduzi dhidi ya KVZ alipata majeraha na kutolewa nje baada ya kugongana na mchezaji wa KVZ wakati wakiwania mpira wa juu.
Majeraha aliyoyapata Augustine Okrah yalimfanya atolewe nje ya uwanja na kupatiwa huduma ya kwanza na madaktari baada ya damu nyingi kumtoka puani.
Kwa mujibu wa Moses Etutu, ambaye ni daktari wa klabu ya Yanga amesema nyota huyo jana alivunjika mifupa ya pua jambo ambalo lilipelekea kutoka kwa damu nyingi na mwisho wakamkimbiza Hospital kwa matibabu zaidi.
Etutu ameweka wazi kuwa nyota huyo kwasasa anaendelea vyema na huenda akaruhusiwa kutoka hospital kesho baada ya kupata matibabu kwa kina.
“Kwasasa hali yake ni njema kabisa, yuko salama anapata nafuu kubwa sana, aliumia jana wakati wa mechi yetu na KVZ, aligongana na mchezaji mwenzake akapata majeraha ya kichwa, akaumizwa upande wa mbele wa fuvu”.
“Tulipofanya baadhi ya vipimo tukagundua amevunjika baadhi ya mifupa ya kwenye pua, kwahiyo alipatiwa matibabu, na ameendelea kupatiwa matibabu hadi sasa hivi”.
“Kiafya yuko salama, damu tena haibubujiki kutoka puani na tunatarajia labda kwa kesho anaweza akawa ameruhusiwa kurudi nyumbani kutoka hospitali, lakini Afya yake ni njema kabisa na yuko salama”.
- Moses Etutu, Daktari wa klabu ya Yanga.